
Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2025/26 huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari amesema utaratibu wa kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kwa njia ya mtandao ulifanywa kwa mujibu wa kisheria baada ya kufanya tathmini.
Aprili 24,2025, Lissu alipinga kesi yake ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa Youtube kusikilizwa kwa njia video na badala yake kutaka kesi hiyo isikilizwe kwenye mahakama ya wazi.
Pia Lissu ambaye kwa mara ya kwanza alipanda kizimbani na kusomewa shitaka hilo na la uhaini Aprili 10,2025 alipinga kesi hiyo kuendeshwa kwa njia ya mtandao, kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imepanga Mei 6, 2025 kutoa uamuzi wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kama itasikilizwa kwa njia ya mtandao ama atafikishwa mahakamani.
Johari ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 30,2025 wakati akichangia katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2025/26.
Akichangia mjadala huo, Johari amesema kitendo cha baadhi ya watu kudai kuwa utaratibu wa kuendesha kesi hiyo kwa njia ya kielektroniki ni ukiukwaji wa sheria kimemsikitisha.
Amesema katika Sheria ya Usimamizi wa Sheria na Matumizi ya Sheria kifungu cha 4 kutengeneza kanuni za usikilizaji wa kesi kwa njia ya mtandao nje ya mahakama.
Johari amesema yapo mazingira mbalimbali waliyoyabaini yaliyowafanya waje na uendeshaji wa kesi kwa njia ya kielektroniki nje ya mahakama.
“Mahakama ita-access (tathimini) mazingira yaliyopo siku hiyo na kuona tusikilezeje kesi hiyo, hasa katika mazingira katika mitandao na social media (mitandao ya jamii) zinarushwa habari za ajabuajabu na za kutisha.,”amesema.
Amesema hiyo ni kwa sababu mahakama jukumu lake sio kushauri tu lakini pia ni kuhakikisha kuwa wakati kesi inaendelea na wananchi wengine waendelea na shughuli zao.
Amesema sio shauri linasikilizwa mahakamani lakini kila kitu kimefungwa na barabara zimefungwa na kuwa kifungu cha tano kinaelezea utaratibu (procedure) itakayotumika, na ndicho kilichofanyika Aprili 24 mwaka huu.
“Watu waache upotoshaji, hakuna sheria ya nchi inayovunjwa, yaliyofanyika ni kwa mujibu wa sheria na hata siku nyingine mahakama ita-access (itathimini)na kuona isikilizwe kimtandao ama wazi,”amesema.
Amewataka watu wanaofanya hivyo, waache kwani wanasababisha taharuki wakati Mahakama inajiendesha hivyo kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu hoja ya Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Vuai Alli Nahodha aliyesema baadhi ya mikataba inachukua muda mrefu, Johari amesema ni kweli ipo mikataba imechukua muda mrefu.
Amesema ni kawaida ya mikataba mikubwa na ya kimkakati kuchukua muda mrefu hasa katika miradi mikubwa kama wa Mchuchuma na Liganga na wa Kusindika Gesi Asilia (LNG).
Amesema hiyo ni kwa sababu kila upande unataka kuhakikisha kuwa una masilahi katika mikataba inayosainiwa.
Bunge limeridhia makadirio hayo yaliyowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndombaro ambaye aliomba limuidhinishie Sh687.69 bilioni huku Sh162.23 bilioni kati ya hizo zikiwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.