
Rome. Taarifa kutoka Vatican imesema hali ya kiafya ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis imezidi kuimarika na alipata usingizi usiku wa kuamkia leo Alhamisi Machi 6, 2025.
Taarifa ya Vatican kwa umma imesema kuwa baada ya kuamka, Papa Francis anayetibiwa maradhi ya upumuaji kwenye Hospitali ya Gemelli mjini Roma aliendelea na matibabu yake, yakiwemo mazoezi ya mwili (motor physiotherapy).
Kama ilivyopangwa, baada ya kutumia mashine ya kusaidia kupumua usiku wa kuamkia leo, alirejeshwa kwenye tiba ambapo asubuhi ameanza kupumua kwa kutumia mipira ya pua (nasal cannulas).
Kama ilivyoripotiwa, Papa Francis anaendelea na baadhi ya shughuli za kikazi.
Taarifa hiyo ya Vatican imesema Alhamisi Machi 6, 2025, Papa Francis alimteua Askofu, Ángel Francisco Caraballo Fermín kuwa Askofu Mkuu wa Cumaná, Venezuela na Askofu Ángel Román Idígoras kuwa Askofu wa Albacete, Hispania.
Papa Francis amekuwa akipokea matibabu ya nimonia ya mapafu yote mawili (bilateral pneumonia) katika Hospitali ya Gemelli huko Roma tangu alipolazwa hospitalini hapo Februari 14, 2025.
Nimonia hiyo inaendelea kumsumbua kiongozi huyo (88), japo madaktari wanaomtibu wameendeleza uangalizi wa kina juu ya afya yake. Papa anashirikiana kikamilifu na tiba anazopewa na hali yake ya moyo inaendelea kuwa nzuri.
Kwa mujibu wa Vatican, madaktari wa Papa wamesisitiza kutokuwepo kwa matatizo yoyote makubwa ya kupumua katika siku mbili zilizopita, japo bado muda unahitajika kwa ajili ya tathimini zaidi.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.