Dar es Salaam. Miezi michache iliyopita, Mwananchi iliripoti hali ya kiafya ya Meneja wa msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ aliyekuwa akisumbuliwa na presha na kupooza miguu. Hata hivyo kwa sasa Fella amesema afya yake imezidi kuimarika.
Fella amesema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo, alikata tamaa ya kupona lakini kwa sasa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani anaendelea vizuri.

“Nina furaha kwani kwa sasa naendelea vizuri, hali yangu inaimarika kila siku na nimeanza kufanya mazoezi ya kutembea kila ifikapo jioni.
“Ukweli mimi nimeumwa sana yaani nimeumwa kweli hadi nikawa nimekata tamaa ya kupona, ila namshukuru Mungu sana hadi sasa naweza kuongea na wewe hivi na kutembea vizuri kwa kufanya mzoezi, ilikuwa balaa,” amesema Mkubwa Fella.

Taarifa za kuumwa kwa Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii kuwa amepoza miguu huku wengi wakidai Diamond amemtelekeza.
Hata hivyo baada ya kupata taarifa hizo Mwananchi ilimtafuata nyumbani kwake Mbagala kata ya Kilungule, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake ambao walidai hali yake haikuwa nzuri hata kuzungumza na mtu kwa muda mrefu.