
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili kutokana na hali ya afya ya hakimu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa ofisa Tehama wa gereza hilo, Sibuti Nyabuya na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, mkazi wa Mbezi.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mwandamizi Godfrey Mhini ilipangwa kuendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashitaka leo Jumanne, Mei 14, 2025 na kesho Jumatano Mei 15.
Shauri lilipoitwa, mwendesha mashitaka Wakili wa Serikali, Edgar Bantulaki ameieleza mahakama wana mashahidi wanne na wako tayari kuendelea na usikilizwaji. Wakili wa utetezi nao pia walikuwa tayari kwa hatua hiyo.
Hata hivyo, Hakimu Mhini amesema hajihisi vizuri kiafya na kwamba, kama binadamu hawezi kuendelea na usikilizwaji.
Badala yake amesema anataka kwenda hospitalini kupata matibabu kwa kuwa afya ni jambo la msingi.
“Kwa hiyo hatutaweza kuendelea leo, kwa sababu hiyo nitaiahirisha tutaendelea kwa tarehe nyingine,” amesema.
Hata hivyo, kabla ya kuiahirisha mashahidi wameitwa mbele ya Mahakama kwa ajili ya utambuzi na kuelekezwa watatakiwa kufika mahakamani kwa tarehe itakayopangwa.
Mashahidi waliofika mahakamani ni Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Juliana Dafi, Mkaguzi Msaidizi Lusekelo Mwanjati, Mkaguzi Msaidizi Asha Mvungi na Kamishna Msaidizi George Wambula, ambaye wakili Bantulaki amesema alitarajiwa kufika mahakamani kesho Mei 15.
Shauri hilo limeahirishwa na kupangwa kuendelea Juni 10 hadi 12, 2025.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi washtakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu wenye asili ya China, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya yanayohusu nyara za Serikali.
Wanadaiwa Desemba 21, 2022, Mkama na Nyabuya walitengeneza nyaraka ya kughushi yenye kichwa cha habari: Nyongeza ya msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru.
Barua hiyo ya Desemba 21 mwaka 2022, ilionyesha kwamba imesainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Kaspar Mmuya ikieleza wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya waliopewa msamaha na Rais.
Ingawa wafungwa hao walitekeleza sharti la kulipa Sh45 milioni, hawakuwahi kutolewa gerezani hadi mmoja wao alipotembelewa na wakili wake akamuonyesha barua hiyo, ambayo alipoifuatilia ilibainika kuwa imeghushiwa.
Shahidi wa kwanza, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha huduma kwa wafungwa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza nchini, Boid Mwambingu ameshatoa ushahidi wake.
Aliieleza Mahakama kuwa Juni 16, 2023, aliitwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mzee Nyamka (wakati huo), akamweleza kuna wafungwa watatu raia wa China wameleta malalamiko wakitaka kuonana na balozi wao nchini.
Alisema Kamishna alimweleza wafungwa hao walimpelekea malalamiko kadhaa dhidi ya Mkuu wa Gereza la Ukonga kwa wakati huo (mshtakiwa Mkama), yakiwamo ya kupewa msamaha na Rais wa kutoka gerezani.
Kamishna alimtuma kwenda kusikiliza malalamiko hayo kwa kukutana nao na mlalamikiwa (mshtakiwa Mkama).
Mwambungu alisema alikutana na wafungwa hao wakamweleza malalamiko yao na alipokutana na Mkama akamuonyesha barua ambayo alibaini haikufuata taratibu za msamaha kwa wafungwa.
Alibainisha kuwa Rais anatoa barua ya kibali ambacho kinakwenda kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye atasaini kibali na kisha atakituma kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, ambaye atakituma kwa wakuu wa magereza wa mikoa husika ambao watakipeleka kwenye vituo husika (gereza) kwa ajili ya utekelezaji.
Shahidi huyo alieleza barua aliyoonyeshwa na Mkama ilikuwa haijakidhi vigezo kwa sababu kibali kilikuwa kimesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, badala ya waziri wa wizara hiyo.