
Mbeya. Mkazi wa Mapelele jijini Mbeya, Evaristo Mwakyoma (69) amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa jirani yake mwenye umri wa miaka mitano.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Teddy Mlimba, Februari 25, 2025 baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote.
Imeelezwa na mwendesha mashtaka wa Serikali, Rajab Msemu kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Aprili 18, 2024 kwa kumuingilia kimwili mtoto wa jirani yake mwenye umri wa miaka mitano wakati akijua ni kosa kisheria.
Amesema siku ya tukio mtuhumiwa alitumia mbinu mbalimbali za kumlaghai mtoto huyo mpaka alipofanikisha lengo lake la kumlawiti na kumsababishia maumivu makali.
Baada ya ushahidi wa pande zote kutolewa mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali aliomba mshtakiwa apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi mfawidhi, Mlimba amesema kwa mujibu wa kifungu cha 154 cha sheria ya kanuni ya adhabu, Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa Mwakyoma kutumikia kifungo cha maisha jela.
Amesema ametoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kuwaathiri kisaikolojia watoto wadogo kwa kuwaingilia kimwili na kuwalawiti.
Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, aliomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa hilo ni kosa lake la kwanza, jambo ambalo lilitupiliwa mbali.
Baadhi ya wananchi jijini Mbeya wamelaani kuibuka kwa vitendo vya matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto na kuomba Serikali kufanya marekebisho ya sheria kwa watuhumiwa wa makosa hayo kunyongwa hadi kufa.
Zainab Hussein, amesema miaka ya sasa wazazi na walezi wamekuwa na hofu kuwapeleka watoto kwenye masomo ya ziada jioni wakihofu watakutana na wabakaji.
“Mitaani hali mbaya, tunaomba Serikali ichunguze na kuwachukulia hatua wazazi wa watoto wanaofanyiwa ukatili na kesi kumalizikia majumbani, hali ambayo inasababisha jamii kushindwa kupaza sauti kufichua ukatili wa kijinsia.