Afrika yachochewa kuwa na sauti moja kuongeza tija zao la kahawa

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Tatu wa mwaka wa nchi zinazolima kahawa (IACO), Peosper Dodiko amesema kuwepo kwa mkataba wa ushirikiano wa nchi wanachama zinazozalisha kahawa utasaidia kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa kwa nchi za Afrika.

Hiyo ni kutokana na nchi hizo kuwa na sauti moja ya ufanyaji biashara na kuchagua kufanya vitu vinavyoweza kukuza uzalishaji kabla ya kuangalia masoko ya nje.

Ametoa kauli hiyo katika siku ya pili ya mkutano wa tatu wa nchi 25 wazalishaji wa kahawa katika Bara la Afrika.

Katika mkutano huo, zinajadiliwa fursa zilizopo na namna ambayo vijana wanaweza kujumuishwa katika sekta ya kahawa.

Dodiko amesema makadirio yanaonyesha kuwa hadi mwaka 2050 kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya kahawa katika soko la dunia na Afrika kwa ujumla hivyo ni vyema hatua kuchukuliwa sasa.

“Kwa ujumla kuna wakulima ambao wanatamani kunufaika na sekta ya kahawa katika masoko ya kimataifa bahati mbaya tumekuwa tukitumia asilimia ndogo ya kahawa inayozalishwa katika nchi zetu hivyo uwepo wa mkataba ni hatua muhimu,” amesema.

Kutotumia kahawa ndani ya nchi hizi umefanya kahawa nyingi inayouzwa nje kuwa ghafi na baadaye kurejeshwa katika nchi mbalimbali ikiwa imeongezwa thamani jambo ambalo hutumia fedha nyingi zaidi.

Amesema mkataba huo utasaidia nchi wanachama kushirikiana ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao la Kahawa.

“Pia zitatamani kushughulikia changamoto ya bishara ya kahawa na kuboresha mnyororo mzima wa bei ya kahawa kutokana na jitihada zinazofanyika katika sekta hii,” amesema.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia  kujielekeza zaidi katika namna ambazo zinaweza kunufaisha watu waliomo ndani ya sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira na kujumuisha watu wengi katika mnyororo na sekta hiyo.

“Hii ni kwa sababu katika uzalishaji tumekuwa na changamoto ya matumizi ya kahawa ndani ya nchi zetu kila mmoja angetamani kujivunia matumizi ya ndani badala ya kuiuza nje tungenunua wenyewe,” amesema.

Hilo litawezekana ikiwa uwekezaji katika miundombinu ambayo itaongeza thamani kama vifungashio ufungashaji na kuongeza uzalishaji utafanyika ndani ya nchi hizo.

“Tunatarajia kuongeza uzalishaji hasa kama tutajiongeza katika kuongeza thamani. Bila mageuzi hatuwezi kutengeneza fursa za ajira kwa vijana na hili tutahitaji nchi na serikali za Kiafrika kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo,” amesema.