Afrika Kusini imesema, ushahidi iliotoa katika kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) unaonyesha jinsi Tel Aviv inavyotumia njaa kama silaha ya vita, lengo likiwa ni kuifanya Ghaza isibaki kuwa na wakazi Wapalestina kwa kuwamaliza kupitia mbinu ya mauaji ya kimbari na kuwahamisha kwa nguvu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Ronald Lamola amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Pretoria: ‘’ushahidi unaonyesha bila shaka yoyote kwamba vitendo vya mauaji ya kimbari vya Israel vina nia maalumu ya kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza. Ni kwa kushindwa kuzuia mauaji ya kimbari, kuchochea mauaji ya kimbari na kushindwa kuwaadhibu wale wanaochochea na kufanya mauaji ya kimbari’’.
Lamola amesisitiza kuwa nchi zote duniani zina jukumu la kuzuia na kutoa adhabu kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari.
Maelezo yenye ushahidi wa kina yaliyowasilishwa na Afrika Kusini kwa ICJ mnamo Oktoba 28 yamedhihirisha wazi jinsi utawala dhalimu wa Israel unavyoendelea kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa 1948 kwa kuendelea kuwateketeza Wapalestina wanaoishi Ghaza kwa kuwaua kimwili na kuwanyima fursa ya kupata misaada ya kibinadamu.

Afrika Kusini imebainisha pia kwamba, Israel inapuuza na kukaidi kutekeleza hatua kadhaa za muda zilizoamriwa na ICJ.
Aidha, Waziri Lamola amesema, Afrika Kusini inalaani uenezaji wa taarifa potofu kuhusu kesi ya mauaji ya kimbari iliyowasilisha ICJ dhidi ya Israel, akisisitiza kwamba, hatua za aina hiyo zinalenga kubabaisha hisia za walimwengu na kuziweka mbali na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa huko Ghaza.
Afrika Kusini iliwasilisha kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya utawala wa Kizayuni Israel katika mahakama hiyo iliyoko The Hague mwishoni mwa 2023, ikiishutumu Tel Aviv, ambayo inaendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Ghaza tangu Oktoba mwaka jana, kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kulingana na Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa 1948.
Nchi kadhaa zikiwemo Uturuki, Nicaragua, Palestina, Uhispania, Mexico, Libya na Colombia zimejiunga na kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa hadharani mwezi Januari…/