Afrika Kusini yachukua hatua baada ya watoto 22 kufa kwa sumu

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameamuru kuondolewa dawa hatari za kuua wadudu barabarani na madukani kama moja ya hatua za kuzuia kuenea sumu ya chakula ambayo iliua watoto 22 hivi karibuni.

Katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni, Rais Ramaphosa amesema: “Tangu mwanzoni mwa Septemba 2024, kumeripotiwa matukio 890 ya magonjwa yatokanayo na chakula katika majimbo yote.” 

Ameongeza kuwa, watu kadhaa wameugua sana na hata kufa baada ya kula chakula kilichoingia sumu ambacho kawaida hununuliwa kwenye maduka ya spaza yaani maduka madogomadogo yasiyo rasmi yanayoendeshwa na wachuuzi wa mitaani.

Mwezi uliopita, Afrika Kusini ilirekodi tukio kubwa la sumu katika kitongoji cha Naledi cha Soweto karibu na Johannesburg, ambapo watoto sita walikufa baada ya kununua vitafunio kwenye maduka ya spaza. Mtoto wa miaka sita ndiye aliyekuwa na umri mdogo zaidi kati ya watoto hao. 

Rais Ramaphosa amesema kuwa, baada ya kufanyika uchunguzi wa kisayansi imebainika kuwa, vifo vya watoto hao sita vimehusiana moja kwa moja na kemikali hatari sana inayotumika kama dawa ijulikanayo kwa jina la Terbufos na ambayo hutumika kuulia vijidudu mashambani na ina madhara hata kwa viwango vya chini kabisa.