
Ofisi ya rais wa Afrika Kusini imetangaza ziara ya Volodymyr Zelensky mjini Pretoria siku ya Alhamisi, Aprili 24. Mkutano huu kati ya marais hao wawili umekuwa ukitarajiwa kwa miezi kadhaa. Ulipaswa kufanyika mapema kidogo mwezi wa Aprili lakini umeahirishwa. Rais wa Ukraine anaiona Afrika Kusini kama nchi ya upatanishi, isiyofungamana na upande wowote, mwanachama wa BRICS na yenye uhusiano wa moja kwa moja kwa Kremlin.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Johannesburg, Valentin Hugues
Katika wiki hii, Afrika Kusini inazungumza na Urusi na Ukraine. Siku ya Jumatatu, mazungumzo ya simu yalifanyika kati ya Cyril Ramaphosa na Vladimir Putin. Rais wa Ukraine anatarajiwa mjini Pretoria leo Alhamisi. Ingawa Afrika Kusini haikushutumu uvamizi wa Urusi mnamo mwezi Februari 2022 na ni sehemu ya BRICS na Urusi, inajaribu kujiweka kama mpatanishi. Ni moja ya nchi chache ambazo zinaweza kuzungumza na Kyiv na Moscow.
Leo, lengo kuu kwa upande wa Afrika Kusini kwa hiyo ni “kuendeleza juhudi za kujaribu kutatua mzozo huo kwa amani,” inaeleza ofisi ya rais. Kwa Ukraine, pia ni nia ya kuimarisha uhusiano wake na nchi hiyo na kuomba kuhusika zaidi, haswa katika kurejea kwa maelfu ya watoto wa Ukraine waliopelekwa nchini Urusi tangu kuanza kwa vita. Mada hii mara nyingi huwa kiini cha mijadala kati ya nchi hizo mbili.
Kwa ujumla zaidi, Ukraine pia inajaribu kusogea karibu na bara laAfrika. Mnamo mwaka 2023, Cyril Ramaphosa alitembelea Kyiv na viongozi wengine kadhaa wa Kiafrika. Mkutano kati ya Volodymyr Zelensky na Cyril Ramaphosa umepangwa kufanyika asubuhi katika ikulu ya rais mjini Pretoria.