
Afrika Kusini imekumbwa na wimbi la baridi kali na hali ya hewa kali tangu mwishoni mwa juma lililopita wakati wa majira ya baridi kali kusini mwa nchi hii, huku theluji ikinyesha na mafuriko makubwa. Mafuriko haya yalikuwa mabaya katika eneo la Eastern Cape, kusini mashariki mwa nchi. Idadi ya vifo vya muda imefikia 49, wakiwemo watoto kadhaa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Dhoruba hii ya msimu wa baridi iliathiri haswa eneo lililo karibu na mji wa Mthatha. Basi dogo la shule limesombwa na mafuriko. Ilikuwa imebeba watu kumi na watatu: wanafunzi sita wameangamia, pamoja na dereva na msaidizi wake, na wanne hawajulikani waliko, anaripoti mwandishi wetu wa Johannesburg, Claire Bargelès.
Manusura kadhaa waliokolewa baada ya kukimbilia juu ya paa au kwenye miti. “Mvua zisizokwisha, upepo mkali, na maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vya watu kadhaa na kusababisha uharibifu mkubwa,” anasema mkuu wa serikali ya eneo hilo, Oscar Mabuyane. Mamia ya watu wamelazimika kupewa hifadhi katika makazi ya dharura baada ya nyumba zao kujaa maji.
Mvua kali
“Hatujawahi kukumbwa na maafa kama haya, lakini sasa, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la joto duniani, hayaepukiki,” ameongeza Oscar Mabuyane, ambaye anasikitishwa na ufinyu wa uwezo uliopo katika mkoa wake wakati shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea, akisikitika kuwa ni helikopta moja pekee inayopatikana kwa eneo zima.
Mvua kubwa za siku chache zilizopita, ambazo pia zimesababisha maporomoko ya ardhi, zimelazimu mamia ya familia kuacha nyumba zao na kusababisha “uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu,” ameongeza.
Siku ya Jumanne, watoto watatu waliokolewa baada ya kukaa kwa saa nyingi kwenye miti ili kuepuka maji yanayozidi kuongezeka, mamlaka imesema. Mamia ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao tangu Jumatatu, haswa kutoka wilaya za OR Tambo na Amathole, ambapo baadhi yao wamehamishwa katika shule na majengo ya serikali ya eneo hilo.