Afrika Kusini kuwasilisha hati ya kina katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutoa ushahidi wa kisayansi kuthibitisha mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
Duru za kidiplomasia zimeripoti kuwa Afrika Kusini leo inatazamiwa kuwasilisha kumbukumbu ya hati ya maandishi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa lengo la kuthibitisha kesi yake dhidi ya Israel kwamba utawala huo unatekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Ronald Lamola Mwanadiplomasia wa Afrika Kusini amesema kuwa ripoti ya kumbukumbu hiyo imebeba ushahidi zaidi wa kisayansi unaonyesha kuwa hiyo ni kesi inayobainisha wazi kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni.

Afrika Kusini iliwasilisha kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel katika mahakama ya The Hague mwishoni mwa mwaka jana ikisema utawala huo ghasibu ambao ulianzisha vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza tangu Oktoba mwaka jana, haujawajibika kuchukua hatua za kusitisha vita na mauajiya kimbari kwa mujibu wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948.
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilifanya vikao viwili vya hadhara tarehe 11 na 12 Januari mwaka huu mjini The Hague ikiwa ni sehemu ya kushughulikia malalamiko ya Afrika Kusini dhidi ya Israel kwa tuhuma za kufanya jinai ya mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Kwa kuzingatia mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza, mahakama hiyo iliamua kuwa, Israel inapaswa kuchukua hatua za kuzuia mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kuboresha hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, lakini uamuzi huu haukujumuisha kusimamisha vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza.