Afrika Kusini haina mpango wa kuchukua nafasi ya ufadhili wa VVU , waziri wa afya anasema

Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Aaron Motsoaledi amesema siku ya Alhamisi kwamba serikali bado haijapata ufadhili mpya kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU baada ya misaada ya Marekani kukatwa, na kukanusha ripoti kwamba mpango wake wa VVU umeathirika pakubwa.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Mpango wa kimataifa wa VVU wa Marekani, PEPFAR, ulifadhili takriban 17% ya bajeti ya VVU ya Afrika Kusini hadi Rais Donald Trump alipokata misaada muda mfupi baada ya kuingia madarakani.

Siku ya Jumatano shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba upimaji wa virusi vya HIV tayari umepungua kwa kiasi kikubwa nchini Afrika Kusini tangu kupunguzwa kwa ufadhili, katika hatua ambayo wataalam wanasema ni ishara tosha kwamba mfumo wa afya uko chini ya shinikizo.

Motsoaledi amekiri  baadhi ya matatizo, lakini amesema haiwezekani kuwa mpango wa VVU wa Afrika Kusini unaweza kuanguka na kushutumu vyombo vya habari kwa kueneza ujumbe hasi.

“Kama upimaji umepungua… tutajaribu kushughulikia, lakini hatufikirii kuwa ni janga,” amesema.

Mara baada ya kuwa kitovu cha kimataifa cha mgogoro wa VVU/UKIMWI, Afrika Kusini imepata maendeleo makubwa katika kupunguza visa na vifo katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Hata hivyo, inaendelea kuteseka zaidi kutokana na VVU duniani, huku mmoja kati ya watu wazima watano akiishi na virusi hivyo.

Fedha za Marekani zimesaidia kulipa mishahara ya wafanyakazi wa afya zaidi ya 15,000, takriban 8,000 kati yao ambao wamepoteza kazi, Motsoaledi amesema.

“Siwezi kuthubutu kusema kuwa tuna mpango kwa watu hawa 8,000, zaidi ya kuzungumza tu na wafadhili na Hazina yetu wenyewe, ambao bado hawajajibu,” amewaambia waandishi wa habari.

Maoni yake yamekasirisha wafanyakazi wengi wa afya, ambao wamekuwa wakisema kwa wiki kadhaa kwamba serikali haichukulii upotezaji wa ufadhili kwa uzito wa kutosha.

Wanaharakati wa VVU walivuruga kikao cha bunge mjini Cape Town siku ya Jumatano katika maandamano, wakitaka serikali kuweka mpango wa dharura.

“Waziri wa Afya anakanusha, na kwa mara nyingine, Afrika Kusini italazimika kukabiliana na matokeo mabaya ya afya ya umma, sio tu ya utawala wa Trump, lakini pia ya kushindwa kwa serikali yetu wenyewe kupanga vya kutosha kwa miezi kadhaa, ” amesema Fatima Hassan, mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la Health Justice Initiative nchini Afrika Kusini.

Motsoaledi amesema serikali imepiga hatua mwaka huu katika kampeni yake ya “Close the Gap”, kwa kuwaweka wagonjwa 520,700 wa VVU kwenye matibabu ya kurefusha maisha kati ya lengo la milioni 1.1 ifikapo mwisho wa mwaka 2025. Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati wametilia shaka takwimu hizo.

“Taarifa tulizonazo haziungi mkono madai haya,” Fatima Hassan amesema. Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha habari hii kwa kujitegemea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *