Afariki dunia baada ya kujirusha chini ya uvungu wa gari

Kahama. Mwanaume ambaye jina lake halikufahamika, amefariki dunia baada ya kujirusha chini ya uvungu wa gari la mizigo, mali ya kampuni ya CIMC.

Ajali hiyo ilitokea kwenye barabara kuu ya Kahama kuelekea Masumbwe, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Aprili 7, 2025.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, alithibitisha tukio hilo na kusema kwamba dereva wa gari hilo, Ally Mohammed (41), mkazi wa Dar es Salaam, amekamatwa kwa tuhuma za uzembe barabarani.

Kamanda Magomi alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa dereva hakuzingatia tahadhari ya barabarani, licha ya kuwepo kwa alama za kivuko cha waenda kwa miguu katika eneo hilo.

“Chanzo cha ajali hii ni uzembe wa dereva kutofuata sheria na taratibu za usalama barabarani. Tunamshikilia dereva pamoja na gari lake. Uchunguzi zaidi utakapokamilika, jalada hili litaelekezwa kwa mwanasheria ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Kamanda Magomi.

Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Zacharia Mirembe, alisema mwanaume huyo alionekana akiwa amelala kando ya barabara katika eneo la Shunu, akiwa na tabia ya kuzungumza peke yake na kusema kwamba alikuwa amekula “upako wa Yesu.” Walieleza kuwa walijaribu kumtoa kwenye eneo hilo kwa kumchapa fimbo, lakini aliendelea kurudi barabarani mara kwa mara.

“Alikuwa akisema, ‘niacheni, nimekula upako wa Yesu, namtumikia Yesu wangu.’ Tulijaribu kumsaidia kwa kumchapa viboko, lakini alikataa kusikia na kuendelea na vitendo vyake,” alisema Mirembe.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo siku ilipotokea ajali, saa 11 jioni, mwanaume huyo alipoliona gari la mizigo likikaribia, alijirusha chini ya uvungu wa gari hilo, na akapitiwa na tairi za nyuma, hali iliyosababisha kifo chake.

Mashuhuda walieleza kuwa alikuwa akionekana kama vile amelewa au alikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa, na hivyo hawakuweza kuelewa tamko lake kwa undani.

Katika hatua nyingine, Gazeti la Mwananchi lilizungumza na Boniface Kagoma, Ofisa Muuguzi Kitengo cha Afya ya Akili katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambaye alielezea kuhusu hali ya mtu aliyeonyesha dalili za tatizo la afya ya akili.

Kagoma alisema kuwa matendo ya mtu kujitoa uhai au kusema maneno yasiyoeleweka yanaweza kuashiria tatizo la afya ya akili, ambalo linachangiwa na unyanyapaa wa jamii na familia za wahusika.

“Unyanyapaa unaathiri sana watu wenye matatizo ya akili. Hali hii inachangia kuongezeka kwa matukio ya kujitoa uhai, kwani watu hawa wanakosa msaada wa kisaikolojia na matibabu. Vilevile, jamii nyingi hutafuta tiba baada ya madhara kutokea, badala ya kutoa msaada mapema,” alisema Kagoma.

Kagoma alisisitiza umuhimu wa elimu ya afya ya akili kwa jamii, akisema kuwa kunyanyapaa kunazidi kuzorotesha hali ya watu wenye matatizo ya akili, na kusema kwamba watu hawa wanapaswa kuonyeshwa upendo na msaada kwa kuwasogeza kwenye vituo vya matibabu.

Aliwashauri watu wenye matatizo haya kuzungumza na watu wa karibu, ili kupata msaada wa kisaikolojia na matibabu.

“Jamii inahitaji kubadilisha mtazamo kuhusu afya ya akili. Wakati mwingine mtu anaonyesha dalili za tatizo hilo, lakini badala ya kumsaidia ananyanyapaliwa. Msaada wa mapema unaweza kumsaidia kupona na kurudi kwenye hali yake ya kawaida,” aliongeza Kagoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *