Afande kuzichezesha Singida Black Stars, Yanga leo

Dar es Salaam. Mechi ya kuzindua Uwanja wa Airtel ambayo itakutanisha timu mwenyeji Singida Black Stars na Yanga leo mjini Singida, itachezeshwa na refa Saady Mrope ambaye ni muajiriwa wa Jeshi la Polisi Tanzania.

Refa huyo mwenye cheo cha mkaguzi msaidizi wa Polisi kutoka Dodoma amechezesha mechi sita za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Miongoni mwa mechi hizo sita ni wa Yanga dhidi ya Singida Black Stars ambao ulichezwa Februari 17, 2025 katika Uwanja wa KMC Complex ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mchezo wa kwanza ambao Saady Mrope amechezesha msimu huu ulikuwa ni Ligi Kuu baina ya JKT Tanzania na Azam FC uliomalizika kwa sare tasa, Agosti 28, 2024.

Akachezesha mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Pamba Jiji FC, Oktoba 3, 2024 kisha akachezesha mechi ya Novemba 23, 2025 ambayo Azam FC iliichapa Kagera Sugar bao 1-0.

Desemba 13, mwaka jana akachezesha mechi ambayo Tabora United iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC na alichezesha mechi ambayo Yanga iliichapa Mashujaa FC mabao 3-2.

Sherehe za uzinduzi zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na michezo, huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA.

Burudani mbalimbali zimetayarishwa kabla ya mechi kuu, ikiwa ni pamoja na muziki kutoka kwa wasanii maarufu wa Bongo Fleva, michezo ya asili, na maonesho ya utamaduni. Mashabiki watapata fursa ya kushuhudia historia ikiandikwa kwa mara ya kwanza mkoani hapa.

Kilele cha tukio hili kitakuwa ni mchezo wa kirafiki kati ya wenyeji Singida Black Stars na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC utakaochezwa kuanzia saa 10 jioni.

Mechi hii inatajwa kuwa ya kuvutia kutokana na nafasi za timu hizi katika msimamo wa ligi, ambapo Yanga wanaongoza kwa pointi 58 huku Singida Black Stars wakiwa nafasi ya nne na pointi 44.

Licha ya kuwa mechi ya kirafiki, upinzani baina ya timu hizi mbili umeibua hamasa kubwa kwa mashabiki. Singida Black Stars wanataka kutumia uwanja wao mpya kuonyesha ubabe wao, huku Yanga wakitaka kuendeleza rekodi yao nzuri dhidi ya wapinzani wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *