Adhabu ya viboko yaendelea kupigiwa msumari, madhara zaidi yakitajwa

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na matukio ya watoto kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa kutokana na adhabu ya viboko, wito umetolewa kwa jamii kuacha kuadhibu na badala yake kuadabisha ili kupata matokeo ya kudumu.

Adhabu hiyo inayotumika zaidi shuleni na wakati mwingine nyumbani inatajwa kuwa si tu huishia kumletea maumivu ya kimwili mtoto husika, bali humuathiri kisaikolojia na kumtengenezea hofu badala ya kumfundisha.

Pia inaelezwa hofu hiyo inaweza kwenda hata kwa watoto wengine wanaoshuhudia.

Katika miaka ya karibuni kumekuwa na matukio ya vifo vya wanafunzi vinavyodaiwa kusababishwa na adhabu kali za viboko ambavyo vinatolewa kinyume na mwongozo wa utoaji adhabu shuleni.

Miongoni mwa matukio hayo ni lile lililotokea   Februari 26, 2025 katika Shule ya Sekondari Mwasamba iliyopo wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambapo inadaiwa kuwa Mhoja Maduhu alifariki dunia baada ya kuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake aitwaye Salim Chogogwe.

Mwanafunzi huyo alikumbana na adhabu hiyo baada ya kushindwa kufanya kazi za vikundi iliyotolewa na mwalimu huyo ambapo kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi waliokuwepo eneo la tukio, Maduhu alipigwa fimbo za kichwani na mgongoni kisha kukanyagwa.

Akizungumza leo Mkurugenzi wa C-Sema Tanzania, Michael Mwarwa amesema kutojiamini kwa wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari ni matokeo ya woga unaosababisha na adhabu ya viboko na nyingine zinazotweza utu wao, hivyo kuathirika kisaikolojia.

“Hakuna utafiti wowote wa kisayansi ambao unaonesha mtoto akipigwa au akipewa adhabu ya viboko anakuwa na akili, msikivu na mwenye nidhamu, lakini kuna tafiti za kisayansi zinaonesha mtoto akipewa malezi mazuri, akiadabishwa anakuwa mwenye akili, kujitambua na kujiamini,” amesema Michael.

Mkurugenzi huyo ambaye shirika lake linahusika kupokea kesi za ukatili amesema katika kipindi cha Januari na Februari wamepokea malalamiko 52 yanayohusu ukatili kwa watoto.

“Kupitia namba ya bure ya 116 kazi yetu ni kupoke kesi zinazohusu matukio ya ukatili, kwa upande huu wa watoto katika kipindi cha miezi miwili tumepokea malalamiko 52 yanayohusu ukatili dhidi ya watoto. Aina za ukatili zilizoripotiwa ni kupigwa, kung’atwa na kuchomwa moto sehemu mbalimbali za mwili,” amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) Martha Makalla amesema licha ya juhudi mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya mbinu mbadala za malezi na nidhamu, vitendo vya ukatili dhidi ya wanafunzi na watoto bado vinaendelea kushuhudiwa ndani ya shule nchini, jambo linaloashiria udhaifu katika utekelezaji wa miongozo na sheria zinazosimamia haki za mtoto ndani ya mfumo wa elimu.

“Machi 4, 2025 Tenmet ilipokea taarifa kutoka kwa moja ya wananchi juu ya kuvunjwa mkono kwa mwanafunzi Khudhaifa Salim Hamisi anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Msufini iliyopo kata ya Chamazi wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

“Mwanafunzi huyu alivunjika mkono baada ya kipigo kikali kutoka kwa mwalimu wake. Kwa mujibu wa taarifa, licha ya tukio hilo kuripotiwa katika kituo cha polisi Mbande kilichopo Mbagala wilaya ya Temeke hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka sasa,” amesema Martha.

Mratibu huyo amebainisha kuongezeka kwa matukio hayo pia kunachangiwa na baadhi ya wazazi kutokuwa tayari kuyaripoti matukio ya aina hii katika vyombo vya dola, ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.

“Wazazi wasio tayari kutoa taarifa wamekuwa wakifanya mazungumzo na familia za watuhumiwa nje na utaratibu uliopo kisheria na wakati mwingine wamekuwa wakipokea fedha zinazodaiwa za matibabu au fidia kinyume cha sheria, tunaomba wanaofanya vitendo hivi waache na badala yake watoe taarifa kwa vyombo vya dola,” amesema Martha.

Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Flugence Masawa amesema adhabu za viboko zimekuwa ni moja ya sababu za kuongezeka kwa utoro mashuleni, hivyo Serikali iikomeshe ili kuhakikisha wanafunzi wanabaki shuleni, wanaendelea na masomo na kukamilisha mzunguko wao wa elimu katika ngazi husika bila vitisho vyovyote.

Kufuatia hilo ametaka Serikali iwekeze katika adhabu mbadala zisizotweza utu wala kutishia masilahi ya watoto na wanafunzi kwa ujumla.

“Serikali ifuatilie pia adhabu zingine ambazo sio za viboko lakini ni mbaya na zinatweza utu wa watoto na kuwasababishia maumivu ya muda mrefu ya kimwili, kisaikolojia na kiakili.

“Wizara ya Elimu kupitia ofisi ya kamishna wa elimu iviimarishe vitengo vya udhibiti ubora wa elimu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti ya kutosha, upatikanaji wa vitendea kazi na utolewaji wa mafunzo ya mara kwa mara ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Pia Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia itoe waraka rasmi unaoelekeza walimu wote kuacha matumizi ya adhabu za viboko zilizopitiliza na kuelekeza mbinu mbadala za nidhamu zinazolinda utu na haki za watoto wakati mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Elimu ukiendelea,” amesema.

Machi 6, 2025 Mwananchi ilizungumza na Kamishna wa Elimu, Dk Lwabwene Mutabwa aliyeeleza kuwa kinachofanywa na Serikali ni kufuatilia kwa ukaribu kuhakikisha mwongozo unatekelezwa kama ulivyotolewa.

Kulingana na mwongozo huo adhabu ya viboko vitatu  kwa mwanafunzi inapaswa kutolewa na mwalimu mkuu au mkuu wa shule au mwalimu aliyekasimiwa jukumu hilo na mkuu wa shule, na inapaswa kutolewa kwa utaratibu.

 “Kusema kwamba adhabu ya viboko itaondoka kabisa sio kweli, hilo linaweza kutokea huko siku za usoni lakini tunachofanya ni kuimarisha ufuatiliaji kuhakikisha adhabu hii inatolewa kulingana na mwongozo.

“Ufuatiliaji wetu utaongezeka maradufu, watakaokiuka watachukuliwa hatua. Hakuna kitu muhimu kwetu kama usalama wa mtoto hivyo wanajamii tunapaswa kushirikiana kwa kutoa taarifa pale unapofanyika ukatili ili hatua zichukuliwe,” amesema Dk Mutahabwa.

Kamishna huyo ameongeza kuwa ufuatiliaji huo utaenda kuongezeka maradufu kwa wathibiti ubora wa elimu, akifafanua kuwa wao ndiyo watakuwa wa kwanza kuhojiwa yanapotokea matukio ya ukatili wa wanafunzi shuleni.

“Kama mthibiti ubora upo na shule yako ina kawaida ya kutoa adhabu kali basi wewe hufai, ni lazima kuwe na ufuatiliaji wa karibu kujua kinachoendelea shuleni,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *