
Simiyu/Mikoani. Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimesababisha madhara kwenye daraja wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Hayo yakitokea, katika maeneo mengine nchini wananchi wametakiwa kutorejea maeneo hatarishi, huku viongozi wakijizatiti kutoa elimu kwa umma ili kudhibiti maafa.
Wilayani Maswa mkoani Simiyu mvua imesababisha daraja kufungwa katika Kijiji cha Bugarama, kwenye Mto Nyamli kutokana na kuwa hatarini kubomoka.
Hali hiyo inatokana na udongo unashikilia daraja hilo kusombwa na maji.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Aprili mosi, 2025 na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Wilaya ya Maswa, imesema daraja hilo limefungwa kwa matumizi ya magari na waenda kwa miguu.
Meneja wa Tarura wilayani humo, Justus Lukanga amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha udongo kumomonyoka pande zote bili za daraja.
“Tumeamua kulifunga daraja hili tangu Machi 29, 2025 kutokana na kuhatarisha maisha ya watumiaji. Tumewasiliana na Tarura Mkoa wa Simiyu na makao makuu Dodoma kwa ajili ya kupatiwa wataalamu,” amesema.
Diwani wa Kata ya Bugarama, Jeremia Matondo amesema kufungwa kwa daraja hilo kumeleta athari kubwa kwa wananchi wanaolitumia kwenda kata jirani ya Masela kufuata matibabu kwenye Kituo cha Afya Mwasayi.
“Daraja hili ni kiungo muhimu kwa wananchi wa kata yetu ya Bugarama maana linatuunganisha na maeneo mengine hasa kwenda kupata matibabu katika Kituo cha Afya Mwasayi. Pia linatuunganisha na wilaya jirani ya Kishapu mkoani Shinyanga,” amesema.
Ameiomba Serikali ilifanyie matengenezo haraka daraja hilo kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwani wapo wakulima katani humo, wenye mashamba upande wa pili ambao hawawezi kuvuka mto.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza kuhusu uwepo wa mvua kubwa mkoani humo, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari na viongozi wa ngazi zote za Serikali kutoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na athari za mvua.
Tahadhari Manyara
Wilayani Hanang mkoani Manyara elimu imeendelea kutolewa kwa wananchi kuchukua tahadhari kwa kutorejea maeneo hatarishi yakiwamo yaliyoathiriwa na maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang, Desemba 3, 2023 yaliyosababisha vifo vya watu 89, majeruhi 139 huku mamia wakikosa makazi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Aprili mosi 2025, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almishi Hazali amesema Serikali ipo makini kwa kushirikiana na madiwani na viongozi wa ngazi za chini, kuhakikisha wananchi hawarejei maeneo hatarishi kwa ajili ya kilimo au biashara.
“Tunashirikiana na viongozi wa ngazi zingine za chini kuendelea kutoa elimu, ili wananchi waendelee kuchukua tahadhari hasa katika maeneo hatarishi,” amesema.
Amesema walipokea maelekezo kutoka kitengo cha maafa kilicho Ofisi ya Waziri Mkuu yakiwataka wajadili kuona ni maeneo gani yanakumbwa na athari kipindi cha mvua na kutengeneza mkakati kuyadhibiti.
“Kata ya Endasiwold kuna baadhi ya wananchi wanalima katika eneo linalopita maji, tumekaa vikao na viongozi wao, hasa kipindi hiki cha mvua na kuwataka wasimame kwani wamelima karibu na korongo maji yanakopita.
“Maeneo kama Kata ya Nangwa kuna mashamba ya watu yanaharibiwa na maji, kijiko kitaenda kule ili kuboresha miundombinu maji yasipite na kuharibu mazao ya wananchi na kuhakikisha usalama unakuwepo,” amesema.
Amesema daraja linalotarajiwa kujengwa mji mdogo wa Katesh, litapitisha maji mengi, tofauti na lililokuwepo ambalo lilikuwa dogo na hivyo kufanya athari kuwa kubwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mary Nagu amesema wanatoa elimu kwa jamii, ili wasirejee karibu na maeneo hatarishi.
“Suala hili pia linasimamiwa na Serikali Kuu ambayo imekuwa ikituma wataalamu kila mara kutoa elimu kwa jamii na kuangalia kama kuna dalili ya vihatarishi vyoyote, ili kutoa taarifa kwa wananchi mapema,” amesema.
Mkoani Morogoro
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo kadhaa ya mkoani Morogoro yakiwamo ya Ulanga, Kilosa, Kilombero na Manispaa ya Morogoro, wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari kuepuka madhara ya mafuriko.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Simba amesema mvua ni za wastani na kuna wakati kunakuwa na vipindi vifupi vya jua, hivyo hakuna madhara yaliyojitokeza.
Hali kama hiyo imeelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka na wa Morogoro, Mussa Kilakala.
“Kuna maeneo ambayo miundombinu ya barabara imeharibiwa na mvua za tangu mwaka jana, Serikali bado tunaendelea na mikakati ya kukarabati miundombinu hiyo,” amesema Kilakala.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amewataka wazazi, walezi na walimu kuchukua tahadhari kwa watoto hasa katika kipindi hiki cha mvua ambacho makorongo na mito imekuwa ikijaa maji.
Wanufaika na maji
Jijini Mwanza baada ya wakazi wake wamenufaika na mvua zinazoendelea kunyesha kwa kujipatia maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Hali hiyo inatokana na baadhi ya maeneo jijini Mwanza kupata maji kwa wiki mara mbili, hivyo mvua iliyoanza kunyesha tangu Machi 22, 2025 imewapunguzia adha ya maji.
Baadhi ya maeneo hayo ni Ihyila, Nyakagwe, Bulale na Tambukareli.
Mkazi wa Mtaa wa Ihyila, Juliana Michael amesema wao hupata maji Jumamosi na Jumanne kila wiki na wakati mwingine hayatoki ila mvua iliyonyesha mfululizo imewasaidia kupata maji ya kutumia.
“Wakati mwingine kwa wiki yanatoka mara moja. Kwa hiyo hizi mvua zimetusaidia sana. Tumepata maji ya kutumia majumbani na kufua nguo,” amesema.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika taarifa kuhusu mwenendo wa mvua za masika (Machi hadi Mei) 2025 ilisema mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara).
TMA ilisema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki na mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu.
Mamlaka ilisema mvua za masika zilitarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Machi, 2025 katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria na pwani ya kaskazini na katika wiki ya pili na ya tatu ya Machi, 2025 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki. Ongezeko la mvua linatarajiwa kuwa Aprili, 2025
Pia ilitoa ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa.
Mamlaka ilitaja athari zinazotarajiwa ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka hivyo kuongeza hatari ya mafuriko hususan katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.
Imeandikwa na Samwel Mwanga (Simiyu), Janeth Mushi (Arusha) na Hamida Shariff (Morogoro) na Saada Amir (Mwanza)