ADC yadai kupokea wanachama 50 wa NCCR-Mageuzi, chenyewe chapinga

Shinyanga. Viongozi 50 wa chama cha NCCR-Mageuzi kutoka ngazi za kata, wilaya na majimbo yote ya uchaguzi mkoani Shinyanga wamedaiwa kukihama chama hicho na kujiunga na chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Taifa, Amir Mshindani Ali, amekanusha taarifa hizo, akisema ni viongozi watano pekee waliohama, huku akieleza kuwa na wao  wanatarajia kupokea wanachama wapya kutokana na mgawanyiko ndani ya Chadema.

“Tukitafuta hao viongozi 50 hatuwaoni. Ni viongozi watano tu waliohama. Kwa hali ilivyo, tunatarajia kuendelea kupokea wanachama wengi zaidi kwa sababu Chadema imegawanyika. NCCR-Mageuzi itaendelea kusimama imara,” amesema Ali.

Akizungumza Mei 14, 2025 wakati wa kuwapokea wanachama hao, Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shabani Itutu, aliwapongeza kwa uamuzi wao na kuwataka kushirikiana na chama hicho kuhakikisha kinapata ushindi kwenye uchaguzi ujao.

“Viongozi waliojiunga nasi tayari tumewakabidhi kadi za uanachama na tumewarudisha katika nafasi walizokuwa wakizitumikia. Mwenyekiti wa jimbo atasalia kuwa mwenyekiti, vivyo hivyo kwa makatibu wa wilaya,” amesema Itutu.

Baadhi ya  wanachama waliokihama NCCR-Mageuzi wamesema walichukua hatua hiyo baada ya kubaini chama chao kilikuwa kinafanya kazi kwa masilahi ya chama kingine kisichotajwa.

“Sababu kubwa ya kuhama ni chama nilichokuwa nacho kilikuwa kinafanya kazi nyuma ya mgongo wa chama kingine. Baada ya kugundua hilo, tuliamua kuhama,” amesema William Mahona.

Naye Samson Paul amesema: “Nimehamia ADC ili kutetea haki za wanyonge ambao hawana watu wa kuwasemea.”

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Kata ya Maganzo, Joyce Amos, amewahamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali huku akiwahimiza kutokuwa na hofu ya kufanya maamuzi ya kisiasa.

“Wanawake wenzangu, jitokezeni kwa wingi kuchukua fomu za kugombea. Msihofu kuhama chama iwapo mtaona dhamira yenu kwa wananchi haijatimia,” amesema Joyce.

Kamishna wa ADC Mkoa wa Shinyanga, Saganda Halid, amesema viongozi hao wapya wamepewa maagizo ya kuhakikisha chama kinapanuka kwa kuzingatia maadili.

“Hakikisheni kila kata inakuwa na mgombea udiwani mwenye sifa stahiki, na kila jimbo liwe na mgombea wa ubunge anayekubalika na wananchi,” ameagiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *