
Arusha. Kiu ya kuoa mke mwingine, imemuingiza matatani Godlisen Lema (48), baada ya kudaiwa kuamua kumuua mkewe ili kutimiza haja yake hiyo.
Lema anayeishi kijiji cha Lekitatu, Usariver mkoani Arusha, anadaiwa kumuua mkewe, Esther Massawe (40) kwa kumpiga rungu kichwani.
Tayari Lema anashikiliwa na Polisi kwa tukio hilo analodaiwa kulifanya Novemba 9, mwaka huu, saa 12 asubuhi nyumbani kwake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, baada ya kutenda tukio hilo, Lema aliufungia mwili wa marehemu chumbani kwake na kwenda kujisalimisha kituo cha Polisi cha Usa River.
Akizungumzia hilo leo Jumatatu, Novemba 11, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mount Meru.
“Hadi sasa tunamshikilia mtu mmoja ambaye ndio huyo mume wa marehemu (Lema) kwa uchunguzi zaidi baada ya kuja kituo cha polisi Usa River kujisalimisha na kukiri kutenda kosa la mauaji.
“Uzuri tulikwenda hadi kwake na kutuonyesha jinsi alivyotekeleza na silaha aliyotumia na vyote viko polisi,” ameeleza.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Mtaa wa Lekitatu, Daudi Mungure amesema kwa mara ya kwanza aliarifiwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Usa River saa 12:40 asubuhi.
“Akaniuliza kama nafahamu nikamjibu sijui, ndio akaniambia tukutane eneo la tukio na nilipofika akaniita kwenye gari kumtambua mwanaume huyo kama mwananchi wangu, nikamtambua ndio akashuka akiwa chini ya ulinzi na kufungua mlango kutupeleka hadi chumbani alikosababisha mauaji hayo,” amesema.
Walipofika ndani, anadai waliukuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha matatu kichwani.
“Katika kumuuliza mtuhumiwa alisema amempiga na rungu kabla ya kwenda kutuonyesha alipolitupa kwenye banda la ng’ombe,” amedai Mungure.
Amesema mwili wa marehemu ulistiriwa, kisha polisi waliondoka na mtuhumiwa na rungu kama kidhibiti kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, Mungure amesema kwa muda mrefu wenza hao walikuwa na ugomvi, kiasi cha kupelekana mahakamani kudaiana talaka.
Mzizi wa yote kwa mujibu wa Mungure, ni kiu ya Lema kuoa mke mwingine na waliposhindwa mahakamani, mume akataka kuuza shamba.
“Nimesikia huyu mtuhumiwa amepeleka kesi mahamakani mkewe ampe talaka, lakini akashindwa,” amedai.
Baada ya kushindwa kesi, Mungure amedai mwanaume huyo aliamua kugawa siku za kulala kwa mkewe na mwanamke aliyetaka kumuoa.
“Akawa analala siku tatu huku na kule analala siku hizo hizo kabla ya jana kuitwa na kuambiwa juu ya tukio hili na waligombana akitaka kuuza shamba kwa ajili ya kumhudumia mwanamke huyo wa nje,” amedai Mungure.
Uzazi ni sababu nyingine
Sambamba na sababu nyingine zilizotajwa, rafiki wa karibu wa marehemu, Merry Nyiti amedai mzizi wa ugomvi wa wawili hao ni uzazi.
Amedai mwanamke alipozaa mtoto wa kwanza ilishindikana kupata mwingine, ndipo mwanaume alipoamua kwenda kwa mwanamke mwingine.
Sakata la mahakamani, amedai lilitokana na mwanaume kudai talaka na mgawanyo wa mali na hapo ndipo Esther aliporidhia mumewe aoe mke mwingine bila kuachana.
Kwa mujibu wa Merry, shemeji yake amezaa watoto wawili na mwanamke huyo mwingine, lakini bado mwanaume alishinikiza kugawanywa kwa mali.
“Marehemu alikataa hilo la kuuza eneo na nadhani ugomvi ukaanzia hapo hadi kusababisha tukio hili,” amesema.
Damu nyingi zimeshuhudiwa eneo la tukio na mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha upande wa sikio, kisogoni na kwenye paji la uso.
“Inaonekana alipigwa akiwa usingizini, maana hana makovu maeneo mengine ya mwili kama aliyejitetea na akaongezewa kwenye paji na kugeuzwa kisogoni maana kote kulivimba na kupasuka huku kunavuja damu,” amesema.
Kaka wa mtuhumiwa, Joshua Lema amesema aliufahamu ugomvi wa ndugu yake na mkewe na kwamba mwanamke mwingine hawamtambui.
“Sisi tunasikia tu fununu lakini hata hatumjui, kikubwa tunalaani tukio hili ni la kikatili na halipaswi kufumbiwa macho,” amesema.
Jirani wa marehemu, Evance Muria amesema tukio hilo ni funzo kwa wanandoa wengine kuwa makini na wenza wao.
“Usiseme nina watoto naye au nimejenga naye au nimetafuta naye chochote, hivyo siondoki hapa, ni heri kuondoka ukiwa mzima kuliko kuondoka ukiwa maiti,” amesema.