Adaiwa kujiua kisa kuambiwa mtoto aliyekuwa akimtunza siyo wake

Njombe. Kijana Justin Mbaga (28) mkazi wa Mtaa wa Kisingile katika Halmashauri ya Mji wa Makambako wilayani Njombe amefariki dunia, kwa kudaiwa kunywa sumu baada ya kuambiwa mtoto ambaye amekuwa akimuhudumia siyo wa kwake.

Akizungumza wakati wa mazishi rafiki wa karibu wa marehemu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Abednego Ngulo amesema Jumapili ya Februarii 9,2025 Mbaga (sasa ni marehemu)  aliitwa nyumbani kwa wazazi wa binti aliyekuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.

Ngulo amedai alipofika nyumbani hapo ndipo aliambiwa kuwa mtoto ambaye amekuwa akimuhudumia toka mama yake akiwa mjamzito mpaka sasa akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu sio wake.

Amedai baada ya kupokea taarifa hizo Mbaga alichukua uamuzi wa kunywa sumu na baada ya kupata taarifa walimchukua na kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu, lakini jana amepoteza maisha.

“Walikuwa wanaishi wote Dar es Salaam mpaka akapata ujauzito jamaa akalea na kuendelea kuishi naye mpaka wanarudi Makambako, lakini juzi kati tuliitwa pale mama yake akadai mtoto siyo wa rafiki yangu,” amedai Ngulo.

Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Kisingile Kata ya Kitisi huko Mjini Makambako wakishiriki ibadan ya mazishi ya marehemu Justin Mbaga aliyefariki kwa kudaiwa kunywa sumu baada ya kuambiwa mtoto aliyekuwa akimtunza siyo wake.

Mama mzazi wa binti huyo, Ratifa Kibiki amesema alikaa na binti yake Desemba mwaka jana na kumhoji vizuri kuhusiana na Mbaga ndipo alipoeleza kuwa mtoto huyo siyo wa Mbaga.

Amesema lengo la kumwambia Mbaga kuwa mtoto siyo wake ni kutaka aache kupoteza fedha kwa ajili ya malezi ya mtoto huyo na kukubaliana kurejesha gharama zilizotumika kwa ajili ya malezi ambazo ni Sh850,000.

“Kwa kweli kwenye kikao hicho alikuja na ndugu zake na mimi nikawa na ndugu zangu alipoambiwa jambo hilo wakawa wameridhia, lakini sasa walipokwenda nyumbani kwao kitu kilichoendelea kwa kweli sielewi,” amedai Kibiki.

Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kisingile, Devotha Nestory amewataka vijana kuacha kutumia hisia katika mapenzi badala yake watumie akili ili kuacha kuchukua hatua ambazo zitakatisha ndoto zao.

“Kuna namna ya ‘kuhandle’ mapenzi au mahusiano kuna wanaotumia hisia na wale wanaodhibiti mahusiano kwa akili nachoweza kuwaasa wajitahidi kutoishi kwa misisimko au mihemko ya mahusiano” amesema Nestory.

Diwani wa Kata ya Kitisi, Navy Sanga amesema kijana huyo amepoteza maisha katika umri mdogo na kumuacha mama yake kutokana na jambo la kupita na huenda angesikiliza ushauri wa wazee asingechukua maamuzi hayo.

“Kijana kaondoka kamuacha mama yake kwasababu ya kuchukua maamuzi ya haraka kama angesubiri na kuongea na mama yake lilikuwa jambo la kupita na angepata mwanamke mwingine,” amesema Sanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga alipotafutwa na Mwananchi Digital kuthibitisha kutokea kwa kifo hicho hakuweza kupatikana hivyo jitihada bado zinaendelea.