
Tabora. Mkazi wa Mtaa wa Mkoani Manispaa ya Tabora, Sara Yohana anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 25 anadaiwa kujinyonga kwa kitenge hadi kufariki dunia baada ya kubaini ana ujauzito.
Akithibitisha kutokea tukio hilo kwa njia ya simu leo Jumanne Februari 19, 2025, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi amesema uchunguzi wa awali umeonyesha chanzo cha kifo chake ni mgogoro wa mapenzi baada ya marehemu kugundua ana ujauzito, lakini mwanaume aliyempa hakuwa tayari kuukubali.
“Hii ni baada ya binti kugundua ana ujauzito ambapo mwanaume hakua tayari kwa taarifa hizo,” amesema Mbogambi.
Mpangaji mwenzie na marehemu, Herman Ernest amesema baada ya kuona imefika saa 5 asubuhi ya leo Sara hajafungua mlango ikabidi watoe taarifa kwenye serikali ya mtaa.
“Mimi nimeona sio kawaida yake kuwa mpaka saa 5 asubuhi hajaamka kuanza shughuli zake ndiyo nikaenda kutoa taarifa serikali ya mtaa wetu wa Mkoani,” amesema.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Madula Shabani amesema baada ya kupigiwa simu kupewa taarifa za tukio hilo alifika na kuchukua hatua za kuvunja mlango na hapo ndipo alikuta mwanamke huyo ananing’inia huku kitenge kikiwa kimezungushwa shingoni mwake.
“Nilikua njiani naenda msibani nikapigiwa simu kua kuna dada toka jana alipoingia ndani hajatoka hadi leo, ikabidi niahirishe kwenda msibani niende sehemu ya tukio…kufika nakuta mlango umefungwa nikaita majirani nikauvunja nikamkuta ananing’inia juu,”amesema.
Mjumbe wa Mtaa wa Mkoani, Issa Zaidi amesema baada ya kuvunja na kukuta mwanamke huyo amefariki dunia tayari walichukua hatua za kupiga simu polisi na kusubiri hatua zingine za kisheria.
Naye, Diwani wa Kata ya Kidongo Chekundu, Chiku Mohamedi amesema baada ya kufika katika chumba cha marehemu alikuta nguo nyingi zimesambaa kitandani na chini sakafuni kilikutwa kipimo cha ujauzito.
Mohamed ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kushirikisha jirani au mtu wa karibu juu ya changamoto zinazowakabili badala ya kuchukua hatua mbaya ikiwemo kujitoa uhai.