ACT Wazalendo yaibwaga CCM, ushindi watenguliwa

Kigoma. Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imetengua ushindi wa Chama Cha Mapinduzi katika Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu, Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya kujiridhisha kuwa haukuwa huru na wa haki.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Katoki Mwakitalu, katika hukumu ya shauri la uchaguzi lililofunguliwa na mwanachama wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo) Lovi Lovi.

Lovi ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mtaa huo wakati wa Uchagusi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024 amefungua shauri hilo kupinga mwenendo na matokeo ya uchaguzi huo.

Alifungua shauri hilo dhidi ya aliyetangazwa mshindi wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Hassan Mlai Mashoto.

Mbali na Mlai (mjibu maombi wa kwanza), Wajibu maombi wengine ni msimamizi msaidizi wa uchaguzi Mtaa wa Gezaulole (ambaye ni mtendaji wa Kata ya Gungu na Msimamizi wa Uchaguzi, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji (ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.

Wanachama wa ACT-Wazalendo wakishangilia nje ya lango la Mahakama ya Wilaya Kigoma, baada ya kushinda shauri la uchaguzi wa mwenyekiti wa Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu, Manispaa ya Kigoma Ujiji, lililofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo Lovi Lovi, dhidi ya Hassan Mashoto wa CCM, aliyetangazwa mshindi.

Lovi aliwakilishwa na jopo la mawakili watatu lililoongozwa na Emmanuel Msasa alijikita katika mashauri ya uchaguzi akisaidiana na mawakili, Eliutha Kivyiro na Prosper Maghaibuni, ambao walipambana na jopo la mawakili wa utetezi zaidi ya 20.

Katika shauri hilo, Lovi alikuwa  anapinga mwenendo na matokeo hayo akidai kuwa mchakato wa uchaguzi na uchaguzi wenyewe uligubikwa na ulaghai na ukiukwaji wa kanuni zilizowekwa na hivyo kuifanya kutokuwa huru na wa haki.

Alidai kuwa ukiukwaji huo wa kanuni, Sheria na taratibu umesabisha madhara makubwa kwa kuwa  umemwanyima wananchi haki yao ya Kikatiba ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Alibainisha mambo yanayoufanya uchaguzi huo kutokuwa halali kuwa ni pamoja na kuwepo kwa tofauti ya idadi ya kura zilizopigwa kwa nafasi ya uenyekiti wa mtaa na za wajumbe katika masanduku ya kura.

Pia, alidai kuwa kulikuwa na tofauti ya kura kwenye fomu ya majumuisho ya kura na zilizoko kwenye fomu ya matokeo ya kila kituo.

Hivyo, aliiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi huo ni batili, hivyo imuamuru msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo atangaze uchaguzi ndani ya siku Saba na ndani ya siku 60 uchaguzi mwingine wa nafasi hiyo uendeshwe.

Walalamikiwa katika majibu yao walipinga madai hayo yote huku wakisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki na kwamba, hapakuwa na kasoro yoyote.

Katika kuthibitisha madai yake, aliwaita jumla ya mashahidi watano akiwamo mwenyewe pamoja na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wote walielezea kwa kina matukio ya ukiukwaji yakiwamo kura bandia zilizokamatwa na zilizoingizwa na wasimamizi wa vituo vya kupigia kura.

Walalamikiwa kwa upande wao waliwaita mashahidi wanne waliotoa ushahidi kinzani dhidi ya madai na ushahidi wa mlalamikaji.

Hata hivyo, Mahakama hiyo katika hukumu yake, imetupilia mbali utetezi wa wajibu maombi hukumu ikikubaliana na madai ya mlalamikaji wakati ikijibu zilizoandaliwa na kukubaliwa na pande zote kama mambo yanayobishaniwa yanahitaji kuamuliwa.

Hakimu Mwakitalu katika uamuzi wake amekubaliana na hoja zote na alisema mdai ushahidi wake aliouwasilishwa kwa mdomo ulioungwa mkono na mashahidi wake wengine, ni mzito na kwamba, amethibitisha madai yake yote pasipo kuacha mashaka yoyote.

Mwanachama wa ACT-Wazalengo wakiwa wamembeba juu aliyekuwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa wa Gezaulole , Kata ya Gungu, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Lovi Lovi nje ya lango la Mahakama ya Wilaya Kigoma,  baada ya kushinda shauri la uchaguzi huo dhidi ya Hassan Mashoto wa CCM, aliyetangazwa mshindi.

Amesema anakubaliana na ushahidi huo kuwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura waliingiza kura bandia na kwamba, mpiga kura mmoja alikamatwa akiwa na kura bandia.

Pia, amekubali kwamba kulikuwa na tofauti ya kura kati ya zilizotoka katika vituo vinne ambavyo vilionesha kuwa mgombea huyo wa ACT-Wazalendo alikuwa ameshinda na hesabu ya kura zilizoko kwenye fomu za majumuisho ya matokeo yaliyotangazwa na kubandikwa ambazo zilionesha kuwa mgombea wa CCM alikuwa ameshinda.

Kutokana na ushahidi huo, Hakimu Mwakitalu amesema wasimamizi wa vituo walikiuka kanuni za uchaguzi huo kutokana na matendo waliyoyafanya na kuufanya uchaguzi huo kutokuwa huru na wa haki.

“Ukiukwaji huo wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi umechafua matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na kubandikwa,” amesema Hakimu Mwakitalu na kufafanua;

“Hivyo naona ukweli katika madai na ushahidi wa mwombaji kuwa baada ya kuhesabu kura, matokeo yalionesha amepata kura 303 lakini baada ya majumuisho ya kura yaliyobandikwa, ikaonekana kuwa ana kura 221 tu vituo vyote vinne,” alisema Hakimu Mwakitalu.

Alisema hali hiyo inayoonesha kuwa matokeo yaliyotangazwa na kubandikwa hayakuwa halali.

“Baada ya kujibu hoja hizo zote kwa kuzikubali, kutokana na ukiukwaji huo wa kanuni, ni wazi wananchi Gezaulole walinyimwa haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka kutokana na udanganyifu wa wasimamizi wa vituo,” alisema Hakimu Mwakitalu na kuhitimisha kwa kusema;

“Mahakama hii inatamka kuwa mchakato na uchaguzi wenyewe wa mwenyekiti wa Mtaa wa Gezaulole uliofanyika  Novemba 27 2024  ni batili na ushindi wa mjibu maombi wa pili unabatilishwa na wajibu maombi wanaamuriwa  kumlipa mwombaji gharama.”

Awali Hakimu Mwakitoki alitupilia mbali shauri la kupinga uchaguzi wa mwenyekiti wa Kijiji cha Kagunga lililokuwa limefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia ACT-Wazalendo, Hassan Mikidadi dhidi ya mgombea wa CCM aliyetangazwa mshindi, Sebaya Sebai na wasimamizi wa uchaguzi.

Hakimu Mwakitalu alitupilia mbali madai ya mlalamikaji kutokana na kupishana kwa kiasi kikubwa kwa ushahidi wake na wa mashahidi wake.

Mashauri haya ni kati ya mashauri 51  yaliyofunguliwa na Chama cha ACT- Wazalendo kote nchini katika Mahakama za Wilaya mbalimbali zikiwemo Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma na Kibiti, kupinga matokeo na mwenendo wa uchaguzi huo.