ACT Wazalendo yabeba jahazi muungano wa vyama, vikwazo vyatajwa

Dar es Salaam.  Wakati kikiendelea kushinikiza umoja wa vyama kupinga maovu yaliyofanyika kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, chama cha ACT Wazalendo kimesema kiko tayari kushirikiana na vyama vingine kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Msimamo huo umetolewa leo Februari 11, 2025 na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, ofisini kwake, jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya chama chake kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Kwa mara ya kwanza katika historia, ushirikiano wa vyama vya siasa kwenye uchaguzi mkuu, ulifanyika wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo vyama hivyo vilitengeneza muungano wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).

Ukawa kilileta matokeo makubwa kwa vyama vya upinzani kwani uliwasaidia kuongeza kura za mgombea uraia ambaye wakati huo alikuwa Edward Lowassa, iliongeza idadi ya wabunge pamoja na madiwani.

Hata hivyo, ulikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya wanachama kutokubali kuwaachia wengine baadhi ya majimbo kama walivyokubaliana. Mfano ni Jimbo la Segerea ambapo Chadema ilikataa kumwachia CUF na kusimamisha mgombea, matokeo yake CCM ilishinda.

Akizungumza kwenye mahojiano hayo, Shaibu amesema wako tayari kushirikiana na vyama vingine katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar. Amesisitiza kwamba ni lazima wakae chini pia kwenye nafasi za ubunge na udiwani.

“Ushirikiano huu una masharti, na siyo kwamba tunayatoa sisi, ni masharti ya kihistoria tuliyojifunza kutokana na jitihada za nyuma. Kwanza, ni lazima kila chama kiondoe fahari za kibinafsi, kuona wewe ni mkubwa, huyu ni mdogo.

“Mkijiona kwamba nyote mko sawa na mnaweza kukaa chini kupanga, umoja wa namna hiyo kwenye uchaguzi utafanikiwa,” amesema kiongozi huyo wakati akizungumza na waandishi wa Mwananchi.

Shaibu ameongeza kuwa ni lazima kutanguliza mbele maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya chama kimoja kimoja. Amesema hiyo ni mitihani ambayo lazima vyama vishinde ili vifanikishe jambo hilo.

Amesema baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, ameviandikia barua vyama vyote ambavyo havikutoa tamko la kuunga mkono uchaguzi huo. Amesema wamewaandikia barua Chadema, CUF, ADC na NCCR Mageuzi.

“Hivi vyama, angalau kwa msimamo baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa, wametoa msimamo unaoonyesha kupinga yale yaliyojitokeza,” amesema Shaibu.

Amesema NCCR Mageuzi waliwajibu kwa barua na wamekaa nao vikao vya faragha na kwamba ni mapema kueleza walichokubaliana. Amesema walikaa pia na ADC wakati wenzao wa Chadema na CUF waliwaeleza kwamba wana chaguzi za ndani, hivyo watakaa baada ya kumaliza michakato hiyo.

“Leo nimepokea wito kutoka kwa Katibu Mkuu wa CUF kwamba wako tayari tukae. Mawasiliano na baadhi ya viongozi waandamizi wa Chadema, walitaka kupata muda halafu ndiyo tukae chini,” ameeleza.

Shaibu amesisitiza kwamba lengo la kutaka kukaa pamoja ni kutaka kutoa tamko kali la pamoja kupinga yaliyofanyika kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana. Amesema hilo tamko litakuwa na uzito kuliko tamko la chama kimoja kimoja.

Amesema hatua ya pili ni kuanzisha vuguvugu kubwa la pamoja la umma kupitia mikutano ya hadhara na maandamano.

“Haya mambo yote yatajadiliwa katika vikao hivi na vyama ambavyo vitakuwa tayari na nina imani kwamba muda si mrefu tutaanza kutekeleza mipango hii na Watanzania wataona,” amesema kiongozi huyo wa ACT Wazalendo.

Katibu mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Addo Shaibu akizungumza na waandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communication Ltd wakati wa mahojiano maalumu jijini Dar es salaam.Picha na Said Khamis

Shaibu amesema anaamini jambo lolote ambalo limepangwa kwa pamoja, likatekelezwa kwa pamoja, lina nguvu kubwa zaidi na uthibitisho wa hilo ni katika vuguvugu la kupigania maoni ya wananchi, ikazaliwa Ukawa.

“Nina Imani kwamba Watanzania wengi wanapenda umoja na watatuunga mkono iwapo tutashirikiana kwa pamoja,” amesema.

Mtendaji huyo wa chama amesema itakuwa ni kupoteza muda endapo watakwenda kwenye uchaguzi kwa mazingira ya kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa. Amesema kazi kubwa ni kuhakikisha hali ile haijitokezi tena.

“Kama mazingira yataonyesha hali ni ileile, siyo wajibu wangu kuamua hatua inayofuata ni ipi, inapaswa kuwa ni msimamo wa chama unaotokana na vikao vya uamuzi. Moja ya ajenda itakayojadiliwa kwenye halmashauri ijayo ni mwelekeo wetu kwenye uchaguzi mkuu ujao,” amesema.

Ameongeza kuwa mkutano huo wa halmashauri kuu ya ACT Wazalendo utakuwa wa kwanza tangu ulipofanyika uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo itapokea taarifa ya uchaguzi huo na kutoa mwekeo wa uchaguzi mkuu ujao.

Kuhusu muda uliobaki kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, Shaibu amesema unatosha kufanya mabadiliko ya msingi, kinachohitajika ni msukumo katika kuilazimisha serikali kupeleka mabadiliko hayo bungeni.

Amesema yapo mabadiliko ya kikatiba, kisheria na kikanuni. Amesema mabadiliko ya kikatiba, ni lazima matokeo ya urais yapingwe mahakamani, ni lazima Tanzania iruhusu mgombea binafsi.

“Tunaweza kupeleka hoja ya mabadiliko madogo ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuruhusu mambo haya,” amesema.

Katika mabadiliko ya sheria, amesema katika Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, walipeleka hoja zinazotaka iwepo kauli bayana kwamba wakurugenzi wa halmashauri hawatasimamia uchaguzi, lakini muundo wa sasa imeipa Tume Mamlaka ya kuteua mtu yoyote wanayeona anafaa.

Msimamo wa vyama vingine

Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema mwelekeo wa chama hicho kuhusu kushirikiana na vyama vingine utatolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.

Mnyika amesema Lissu anatarajiwa kuzungumza hivi karibuni, hotuba hiyo ndio itakayotoa maelekezo kuhusu chama iwapo kitashirikiana na vyama vingine au vinginevyo.

“Mwenyekiti wetu atazungumza hivi karibuni (hakutaja lini), katika hotuba hiyo atatoa mwelekeo wa chama kuhusu kushirikiana na wengine,” ameeleza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Abdallah amesema ushirikiano na vyama vingine si miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa katika vikao vya hivi karibuni vya chama hicho.

Hata hivyo, wamepokea wito kutoka ACT Wazalendo, alisema wataamua kwa vikao iwapo washirikiane au la, hasa ukizingatia kuna historia mbaya katika kushirikiana.

“Kama tutashirikiana bila shaka kutakuwa na masharti, siwezi kusema kwa sasa kwa sababu hili jambo linahitaji uamuzi wa vikao, kwa hiyo tukiamua tutakuwa na mengi ya kueleza,” amesema.

Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo amepongeza wazo kutoka ACT Wazalendo, hata hivyo amesema kwa sheria za Tanzania na tabia ya vyama vya siasa, ni jambo ambalo haliwezekani kwani waliona wakati wa Ukawa.

Amesema vyama vya siasa viligombana wakati wa kuachiana majimbo ambapo amebainisha kwamba maeneo mengi ambayo CUF ilikuwa na nguvu, Chadema waligoma kuachia, mfano Jimbo la Segerea na Jimbo la Masasi alikokuwa akigombea marehemu Emmanuel Makaidi.

“Jambo jingine lililowaumiza Ukawa ni namna ya kugawana ruzuku baada ya uchaguzi, kwa sababu kushinda ni hatua nyingine na kushindwa ni hatua nyingine pia. Mkinda mnakwenda kuunda serikali, modality ya muundo wa serikali haipo katika maudhui ya Ukawa.

“Kwa hiyo, mtu anapokuja na hilo wazo, maana yake anakuja kuvishawishi vyama ili anufaike yeye kama walivyonufaika Chadema kwenye Ukawa. Ni wazo zuri lakini halina utaalamu wa namna ya kuliendea,” amesema Doyo.

Mwenyekiti wa TLP, Richard Lyimo amesema wao wanaamini kwamba muungano unaongeza nguvu kwenye mapambano, lakini anahoji mazingira ya muungano yanayopendekezwa kama yatakuwa tofauti na yale ya Ukawa.

“Vyama hivi vya upinzani, wanataka waonekane wameanza kulizungumza hili la muungano, lakini viongozi wenzangu wana unafiki zaidi kuliko uamuzi wao, inakuwa ni vigumu kuamini, ukweli wa muungano uko wapi.

“Muungano naupenda sana lakini ni pale itakapotokea vyama hivi vikawa na jibu la maswali ambayo watu wengi wanajiuliza. Mazingira yaliyopo sasa hivi hayaonyeshi kama vyama hivi vikiungana, vyote vitakuwa na mafanikio,” amesema.

Makamu wa Rais wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini amesema wao hawakatai muungano wala ushirikiano wowote, isipokuwa Sheria ya Vyama vya Siasa hairuhusu muungano wa aina yoyote wa vyama vya siasa.

Amesema ushirikiano uliopita wa Ukawa, ulikwaza baadhi ya vyama kwa sababu makubaliano yaliyofikiwa kwenye vikao vyao ikiwemo kugawana majimbo ya kusimamisha wagombea ulikiukwa. Amesema NCCR Mageuzi walikuwa waathirika wakubwa katika hilo.

“Changamoto ya pili ni kwamba ruzuku inatokana na kura zinazopatikana, ili upate ruzuku lazima upate asilimia 5 ya kura zote. Ushirikiano huo ulifanya vyama vingine visikidhi vigezo hivyo, hauwezi kufanya siasa kama huna nguvu za kiuchumi,” amesema.