
Shinyanga. Ofisa wa oganizesheni mafunzo na uchaguzi kutoka Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Risasi Semasaba amesema kuwa katika Mkoa wa Shinyanga kuna wanachama wanane waliochukua fomu za kutia nia ya ubunge na jimbo la Shinyanga mjini limekuwa na watia nia wengi.
Akizungumza leo Mei 21, 2025 katika hafla fupi ya kufungua uchukuaji fomu za kutia ni ya ubunge na madiwani iliyofanyika mkoani Shinyanga, amewataka wananchi hasa wanawake kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu.
“Waliochukua fomu ni wanachama wanane, wanawake wawili na wanaume sita wengi wanajitosa jimbo la Shinyanga mjini na hatua hii itafungwa Mei 31, 2025,” amesema Semasaba.
Baadhi ya watia nia ya ubunge wameeleza kilichowashawishi kuchukua fomu ikiwa ni pamoja na kuifanya Shinyanga kukua kiuchumi pamoja na sekta ya afya,
“Shinyanga ina dhahabu, pamba, idadi kubwa ya ng’ombe ambao wanasaidia kuzalisha maziwa lakini katika maendeleo bado tuko nyuma, jambo ambalo linahitaji suluhisho,” amesema Sili Yasini.
“Binafsi napenda kufanya kitu ambacho kitanufaisha wengi na naamini nitafanya maendeleo kwa wananchi kama chama kikiridhia kunikabidhi kijiti cha kuwania ubunge” amesema Hassan Ibrahimu.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo jimbo la Shinyanga mjini, Mbaluku Haji amesema kuwa baada ya baada ya hatua hiyo ya uchukuaji fomu wanasubiri mkutano mkuu utaamua ni nani atapeperusha bendera ya chama hicho mkoani humo.
“Hatua hii ya uchukuaji fomu za kutia nia litamalizika Mei 31, 2025” amesema Haji.