ACT-Wazalendo: Hatutaki kuvunja Muungano, tunahitaji usawa

Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema hakina lengo la kuuvunja Muungano, badala yake wanahitaji usawa utakaojenga heshima kwa pande zote mbili za Zanzibar na Tanzania Bara.

Hayo yamesemwa leo, Jumatatu Aprili 14, 2025, na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud Othman, wakati akihitimisha ziara yake ya kuzungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali za chama hicho katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Kiongozi huyo amesema si kosa kwa Mzanzibari yeyote kuhoji muundo wa Muungano kwa sababu ni haki yake ya msingi ya kupambania mabadiliko ili kujipambanua.

“Si kosa, wala si jinai kwa Mzanzibari kuuhoji muundo wa Muungano na kupigania mabadiliko ya kimsingi kwenye Muungano huu. Hilo ni suala la wajibu na haki kuisemea nchi yake. Nanyi nawasihi mjipambanue kwenye hilo,” amesema Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Amesema kupotea kwa heshima na haki ya nchi imekuwa sababu mojawapo ya kushuka kiuchumi.

Akitolea mfano wa mambo hayo, amesema kwa nchi zilizo ukanda wa bahari, suala la kumiliki bandari na ushuru wa forodha ni sehemu adhimu katika kufanya uamuzi wa kisoko na kiuchumi, ila kwa Zanzibar ni tofauti kwa kuwa mambo yote muhimu yapo chini ya mwamvuli wa Muungano.

Pia, mwenyekiti huyo amewataka viongozi wa chama hicho kutambua kwamba matumaini ya Wazanzibari wengi ni ukombozi wa nchi yao na imani, amedai, ipo mikononi mwa ACT-Wazalendo.

“Wapo viongozi katika nchi hii ambao ukiligusa suala la Muungano wanakuwa wakali kana kwamba ni uhaini. Hii ni haki, na mamlaka zinapaswa kutoa ufafanuzi wa kina kwa anayehitaji kutambua,” amesema kiongozi huyo.

Mbali na hilo, Othman amewahimiza viongozi wa ACT-Wazalendo kuendelea kuwamsha wananchi kifikra, hasa wale ambao hawajaielewa dhamira ya safari yao mpya ya ukombozi wa Zanzibar.

Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa, amesema ushindi utakaopatikana baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, si wa ACT-Wazalendo pekee, bali ni wa kuikomboa Zanzibar.

“Katika ushindi huu ambao utakufanya Othman kuwa Rais wa Zanzibar, sisi wananchi kuna mambo ambayo ni kiu yetu kuyapata, ikiwamo kuturejeshea mamlaka yetu ya Zanzibar, kutuunganisha Wazanzibari na kupinga ubaguzi na utengano, kutubadilishia maisha ili kupata vipato vinavyostahili,” amesema Jussa.

Pia, amesisitiza endapo Othman atachaguliwa na chama kikashika hatamu, watafungua fursa za ajira kwa vijana, sambamba na kuyarudisha maono ya Maalim Seif Sharif Hamad ya kuibadilisha Zanzibar kuwa Singapore.

Akitoa salamu zake katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mansour Yusuf Himid, amewataka watawala kuwaachia wananchi uhuru wa kufanya uamuzi wa kidemokrasia bila kuwashurutisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *