Unguja. Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana ya kuwataka wafanyakazi wa serikali katika mkoa huo kuwasilisha kadi za mpiga kura azikague, imevunja sio tu katiba bali sheria tano za nchi. Imeelezwa.
Kitwana alitoa kauli hiyo Aprili 28, 2025 wakati akizungumz ana waandishi wa habari ofisini kwake Vuga ambapo alisema baada ya watumishi kupeleka vitambulisho hivyo ripoti hiyo ataiwasilisha kwa Rais wa Zanzibar Dk Hussein mwinyi yeye ndio atajua hatua za kuchukua.
Sheria zinazotajwa kuvunjwa na mkuu huyo wa mkoa ni pamoja na sheria ya uchaguzi Zanzibar na Tanzania bara, Sheria ya ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2023, Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma na sheria ya utumishi wa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 5, 2025 katika ofisi kuu za Chama cha ACT -Wazalendo, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Omar Said Shaaban amesema kwa mujibu wa sheria hizo alichokifanya mkuu wa mkoa ni cha kihalifu na kosa la jinai huku akiwataka watumishi wasitishwe wala kutiwa hofu na kauli hiyo kwani ajira ni haki zao na siyo hisani, wapo kwa mujibu wa katiba “upo pale kushiriki ujenzi wa nchi yako kutokana na kipaji na elimu uliyonayo.”
“Hii ni kauli ya aibu na kihalifu yenye nia ovu na kuwatia hofu watumishi na viongozi katika mkoa huu wa mjini Magharibi, ni kauli ya kijinai na ukosefu wa maadili na mhemko wa kisiasa, hili kazi anayotaka kufanya ni ya kuhamasisha uhalifu,” amesema Shaaban ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.
Hata hivyo Mwananchi lilipomtafuta Kitwana kuhusu mtazamo wa kuvunjwa kwa sheri hizo na yanayoendelea, amesema msimamo wake upo palepale na kwamba hakusema jambo hilo kwa kukurupuka ila amelisema akiwa anatambua majukumu yake akiwa mkuu wa mkoa.
Katika kufafanua zaidi, amesema tayari viongozi na watendaji wakuu wameshaanza kuwasilisha vitambulisho hivyo na wengine wakimtumia kwa simu avikague.
“Kwa watu wasiojua kazi ya mkuu wa mkoa ndio watasema, lakini hii ni miongozi ma kazi za mkuu wa mkoa, na msimamo wangu upo palepale,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Kitwana amesema kwa kadri inavyoendelea ikimpendeza ataziomba hata wizara na mawaziri wawasilishe vitambulisho hivyo huku akitaja moja faida kwamba ni kujua idadi ya watu waliojiandikisha katika mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana akionesha kitambulisho cha mpiga kura kilichowasilishwa kwake kwa ajili ya kukikagua.
Akifafanua namna sheria hizo zinavyovunjwa, mwanasheria huyo amesema kifungu cha 118 (G) cha sheria ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inaeleza kwamba ni makosa mtu yeyote kuuza, kununua au kumpatia kitambulisho cha kupiga kura mtu ambye hausiki.
Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu akikutwa na hatia atalipa faini kati ya Sh300,000 hadi Sh3 milioni au kifungu cha miezi mitatu hadi miezi sita maanayake ni jinai na mkuu wa mkoa hayupo katika mnyororo wowote unaohusiana na kitambulisho cha mpiga kura.
Amesema hili ni kazi ya kuhamasisha uhalifu hilo ni kuwashawishi watende kosa la jinai kwahiyo anawashawishi wafanye kosa la jinai.
Amesema sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi sura ya 44 ya mwaka 2023 ambayo imeanzisha Tume ya ulinzi binafsi inataka kuhakikisha haki za raia ambazo ni kulinda faragha za mtu.
“Sheria hii imevunjwa kwasababu vitambulisho vilivyotakiwa kupelekwa, inatambua taarifa zote zinatolewa kwa njia ya biometriki, ambazo ni taarifa nyeti za mtu,” amesema Shaaban.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu cha 14 (1) kinapiga marufuku kwa mtu ambaye hajasajiliwa kama mdhibiti wa taarifa kuchukua taarifa binafsi na mkuu wa mkoa hatambuliki na sheria hiyo.
“Tunawasihi viongozi wote wasije wakafanya huu mchezo wakapeleka vitambulisho vyao kwani, hatari ni kubwa maana hawajui baada ya pale nini kitafanyika kuhusu vitambulisho hivyo,” amesema mwanasheria huyo.
Sheria nyingine ni sheria namba nne ya mwaka 2015 ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inawaongoza nini cha kufanya na wapi wasema ambapo ni kuongea mambo yasiyofaa kwenye umma.
Sheria ya utumishi wa umma namba 2 ya mwaka 2011 na sheria namba tatu yam waka 2003 ambayo inaweka misingi ya watumishi wa umma kujihususha na siasa.
Amesema alitumia ofisi za umma cheo cha umma kufanya kazi ya siasa jambo ambalo halikubaliki kwa mujibu wa sheria.
“Niwatoe hofu watumishi na watendaji wote kwamba hawalazimiki kupeleka kitambulisho kwa mkuu wa Mkoa, na wala hawalazimiki kupiga kura kwa maelekezo ya viongozi kwani katiba imetoa uhuru na haki ya kuchagua mtu anayemtaka,” amesema.
Kutokana na hali hiyo Shaaban amesema chama kinazitaka mamlaka husika kuchukua hatua zinazostahiki ikiwemo Tume ya Uchaguzi kutoa kauli na onyo kwa Kitwana na kuwahakikishia wananchi kuwa wanahaki na wajibu wa kupiga kura na vitambulisho hivyo ni mali yao na Mkuu huyo wa Mkoa sio miongoni mwa, wanaostahiki kukabidhiwa vitambulisho hivyo.
“Watoke hadaharani wawatoe wananchi hofu, wawaeleze kuwa mkuu wa mkoa sio miongoni mwa watu aanotambuliwa an sheria kukagua vitambulisho hivyo badala yake wenye mamlka ni Zec na INEC,” amesema Shaaban
Pia, wameitaka Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi kuchukua hatua dhidi ya Kitwana kwa ni taarifa binafsi za watumishi wa Mkoa huo zipo hatarini na kuchakatwa na mtu asiyehusika kwani hakuweka wazi anataka kuzifanyia kitu gani.
Sambamba na hilo, wanaitaka Tume ya Maadili ya viongozi wa umma pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Zena Said, wauchukue hatua za kinidhamu na maadili dhidi ya Kitwana kwa kukiuka misingi ya utumishi wa umma.
Kutokana na jambo hilo kuwa la kijinai, pia chama hicho kimelitaka Jeshi la Polisi la Mkoa huo kufanya uchunguzi juu ya uhalifu unaotaka kutendwa na Mkuu huyo wa Mkoa kisha lichukue hatua dhidi yake.
Wadau wa uchaguzi
Jana Mwananchi lilizungmza na wadau wa uchaguzi ambao nao walionesha kushangazwa na kupinga kitendo hicho akidai kinalenga kuwatia hofu na kuwaelekeza watumishi wa umma cha kufanya wakati wa kupiga kura huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kikijiweka kando na kauli hiyo.
Pamoja na hao, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Joseph Kazi naye alisema mtu anayepewa kadi hiyo ni yake mwenyewe na ni mali ya Tume ndio maana kama mtu akipoteza inarejeshwa tume.
“Mtu anatakiwa akae na kadi yake asimpatie mtu mwingine yeyote na kubwa ambacho naweza kusema masuala ya kujiandikisha na kupiga kura hizi ni haki za wananchi kikatiba na ni haki yeye mwenyewe ana uamuzi wake akiamua kwenda kujiandikisha na ni uamuzi wake kupiga kura, kumchagua mtu anayemtaka na sio suala la lazima,” amesema.
Wengine waliozungumzia jambo hilo ni pamoja na Mwenyekiti Chama cha AAFP Taifa, Said Soud Said alisema kitendo hicho hakikubaliki na ZEC haipaswi kufumbiwa macho.
“Unapowachukua watu kwa maana ya kwamba uwakague, maana yake tayari unawatia ama kutishia ajira zao, ajira ni haki yao lakini unachokitumia wewe unakuwa kama ngao ya kutaka kuwapeleka unapotaka wewe, hii sio haki,” amesema.
Amesema, ZEC haipaswi kulifumbia macho jambo hilo katika mazingira ya kuendeleza demokrasia “sisi kama wanasiasa hatupendi kuona kitu kama hicho, inatakiwa Tume ikemee mambo yanayojitokeza yanayoharibu nia na dhamira ya uchaguzi.”
Naye Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Chama cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, Khamis Mbeto amesema huo sio msimamo wa chama bali ni wa mkuu wa mkoa mwenyewe kwani wao hawatarajii wala kuagiza jambo kama hilo lifanyike kwasababu wanaheshimu misingi ya demokrasia.