Dar es Salaam. Waimbaji wa Bongofleva, Abigail Chams na Harmonize wanaendeleza ushirikiano wao wa kikazi wa muda mrefu na sasa wamekuja na mradi wao mpya ambao unalenga tuzo kubwa zaidi za muziki duniani za Grammy zinazotolewa macho na wengi.
Hatua hiyo inakuja takribani miaka mitatu tangu waandaaji wa tuzo hizo, recording academy kuanzisha kipengele cha muziki Afrika, Best African Music Performance ambacho tayari kimetoa washindi wawili, Tyla na Tems.
Tuzo hizo zilizoanza kutolewa Mei 4, 1959 huko Marekani, wakati huo zikifahamika kama Gramophone, hadi sasa Beyonce Knowles ndiye ameshinda mara nyingi zaidi duniani huku Angelique Kidjo akiongoza kwa upande wa Afrika.
Tangu mwaka umeanza, Harmonize amekuwa akisitiza ukaribu wake wa kikazi na Abigail Chams umekusudia kufanya muziki mzuri na kushinda tuzo na sasa wanajiita ‘grammy gang’ wakiwa tayari wametoa wimbo mmoja.
Kwa sasa wanafanya vizuri na wimbo wao, Me Too (2025) uliotayarishwa na B Boy Beats huku video yake ambayo tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 1.2 YouTube ikiongozwa na Director Kenny, mshindi wa tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA).

Ndani ya muda mfupi wimbo huo umepata mapokezi mazuri, mathalani umeshika namba moja katika chati ya Apple Music Tanzania na kumfanya Abigail Chams kuwa msanii wa kwanza wa kike Bongo kufanya hivyo ndani ya mwaka huu.
“Kutoka kwa msichana anayeishi kwa ajili ya muziki, hii ni ndoto iliyogeuka kuwa kweli kwangu. Ningependa kuwashukuru wote mlioshiriki kwa ukaribu katika safari yangu. Me Too ni wimbo mkubwa zaidi nchini kwenye mitandao yote,” alisema Abigail Chams.
Wimbo huo (Me Too) unakuja ikiwa ni muda mfupi tangu Abigail Chams kuonekana tu katika video ya wimbo mpya wa Harmonize, Furaha (2025) unaofanya vizuri kwa sasa katika majukwaa mbalimbali ya kusikiliza muziki.
Hapo awali, wawili hao walishatoa nyimbo mbili pamoja, kuna Closer (2022) wake Abigail Chams, na Leave Me Alone (2022) unaopatika katika albamu ya tatu ya Harmonize, Made For Us (2022) iliyowania Tuzo za Muziki Tanzania (TMA).
Ikumbukwe Abigail Chams katika safari yake ya muziki alianza kwa kujifunza kupiga piano akiwa na umri wa miaka mitano, alipofikisha miaka minane akawa amejua na violini, gitaa, ngoma na filimbi.
Baada ya kuiva vizuri upande huo, akaanza kurekodi na kuweka kazi zake kwenye mitandao yake ya kijamii na polepole Bongofleva ikampokea na sasa ni miongoni mwa wasanii wa kike wa muziki huo wanaosifika kwa ukali.
Baada ya kuachia wimbo wake, Reimagine (2020) alipata nafasi ya kufanya kazi na shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) Tanzania kama Balozi, pamoja na kutumbuiza kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai. Mwaka 2022 Abigail alisainiwa na menejimenti ya RockStar Africa na baadaye lebo kubwa duniani, Sony Music Entertainment Africa ikasaini mkataba wa kufanya naye kazi na hata mradi wake huu mpya wao ndio wamesimamia.

Baada ya kusaini dili hilo pamoja na wenzake wawili kutokea Tanzania ambao ni Aslay na Young Lunya, Abigail Chams alisema ndoto yake ni kuja kushinda tuzo kubwa kama Grammy na BET zinazotolewa nchini Marekani.
“Malengo yangu ni kupeleka Bongofleva, muziki wa Kitanzania kimataifa zaidi, na sasa hivi natazama tuzo za Grammy, nawaza kuzipata kwa miaka ijayo, kwa sababu ziko hapo kwenye malengo na nina amini nitazipata,” alisema Abigail Chams.
Mwaka huu baadaye Abigail Chams na Harmonize wanaweza kuwasilisha kazi yao kwa ajili ya kupata uteuzi wa Grammy 2026 ambapo wasanii wa Afrika wametanuliwa wigo wa kushinda baada ya kupewa kipengele chao wenyewe.
Ikumbukwe katika tuzo za 67 za Grammy 2025, mwimbaji kutokea Nigeria, Tems ndiye aliyeshinda kipengele hicho kupitia wimbo wake, Love Me Jeje (2024) akiwashinda mastaa kama Asake, Burna Boy, Yemi Alade na Davido, wote kutokea Nigeria pia.
Tems aliyevuma zaidi baada ya kushirikishwa na Wizkid katika wimbo, Essence (2020), amekuwa msanii wa pili Afrika kushinda kipengele hicho baada ya Tyla wa Afrika Kusini kushinda 2024 kupitia wimbo wake, Water (2023).
Angelique Kidjo kutokea Benin ndiye mwanamuziki solo Afrika aliyeshinda tuzo nyingi za Grammy ambazo ni tano, akiwa amepambana na muziki kwa zaidi ya miaka 40 huku akitoa albamu 16 tangu mwaka 1989 hadi 2021 aliposhinda tuzo yake ya mwisho.