Dar es Salaam. Kipaji huwa hakifichiki. Akiwa ndiyo kwanza ana miaka mitatu kwenye sanaa ya muziki, lakini nyota yake imekua kwa kasi na kuwaburuza baadhi ya wasanii walioanza kitambo kwenye game ya Bongo Fleva.
Ana sauti nzuri, anajua kutumia vyombo na anajua kuimba. Kwa kifupi unaweza kusema ni mwanamuziki aliyekamilika kutokana na uwezo huo.
Ametoa nyimbo zinazofanya vizuri nchini na kimataifa kama ‘Me Too’ aliyomshirikisha Harmonize, Muhibu, Chapati, Tucheze ambao ndiyo uliomfungulia nyota na nyingine nyingi.

Hata hivyo, katika soko la muziki kuna mambo ya kuyafanya ili ufikie au upite mafanikio ya baadhi ya wasanii waliokutangulia.
Kwa Abigail kazi ndiyo kwanza imeanza. Safari ya muziki ndiyo kwanza mbichi na anayeangaliwa mbele yake ni Tyla, mwanamuziki kutoka Afrika Kusini.
Kuna wasanii wengi wa Bongo Fleva unaweza kuwaweka level ya juu zaidi yake lakini wengi hawajatoboa kimataifa, hivyo, kwauwezo wa Abigail, ni wazi akifikia daraja Tyla ni moja ya kipimo cha kipaji chake.
Kwa nini Tyla? Amekuja kwa kasi sana. Wimbo mmoja tu wa ‘Water’ alioutoa mwaka 2023, umemtambulisha kimataifa na kushika chati mbalimbali duniani huku akijitambulisha kwa aina za muziki kama Afro Beat, RnB na Amapiano.
Alipata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake ‘Water’ alioutoa Julai 2023, ambao ulienea kwenye mitandao ya kijamii kama TikTok, na kufikia nafasi za juu kwenye chati za muziki nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, Marekani na Uingereza.

Mafanikio ya “Water” yalimfanya Tyla kuwa msanii wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kutoka Afrika Kusini kuingia kwenye chati ya Billboard Hot 100 nchini Marekani tangu Hugh Masekela mwaka 1968.
Wimbo huo uliendelea kufanya maajabu na Tyla alishinda tuzo za Grammy ebruari 2024 katika kipengele kipya cha ‘Best African Music Performance’ kupitia wimbo huohuo, na kuwa msanii mwenye umri mdogo zaidi barani Afrika kushinda tuzo hiyo.
Kwa mafanikio hayo hadi sasa, Abigail ana kazi kubwa ya kufanya kuyafikia na kuyapita lakini kuna mambo kadhaa kama atayazingatia ni wazi safari yake itakuwa nyepesi kumfikia.
Promosheni
Kama ilivyo kwa Tyla, hajatumia nguvu nyingi sana kujitangaza. Kipande kidogo tu cha wimbo ‘Water’ alichokiweka kwenye ukurasa wa TikTok ndiyo kimempa ‘platform’ ya kusikilizwa duniani.
Ingawa wakati mwingine kuna kitu ‘bahati’ lakini hata wimbo wenyewe umeshika kasi kutokana na promosheni baada ya kufanya ‘remix’ ya wimbo huo.
Hata mwenyewe alisema “Mitandao ya kijamii ndiyo imesababisha wimbo wangu ujulikane zaid. Hata mimi mwenyewe sijaamini. Nilipoupakia TikTok haukumaliza hata saa mbili ukafikisha watazamaji zaidi ya milioni moja.”

Hivyo, kwa Abigal mbali na kuingia studio ana kazi kubwa ya kutangaza kazi zake ili ziwafikie wengi duniani kote.
Kama utakumbuka Abigail aliwahi kupostiwa na msanii wa Marekani, Beyonce baada ya kufanya Cover ya wimbo wa msanii huyo mkubwa duniani ‘Brown Skin Girl’ wa mwaka 2020. Hii ilidhihirisha kipaji cha Abigail ambacho kinahitaji promo zaidi ili kizidi kumpa mafanikio.
Kutokukata tamaa
Wapo wasanii wengi wa Bongo Fleva hasa wa kike ambao safari zao za muziki zimepungua au kufika mwisho kutokana na changamoto mbalimbali zikiwamo usimamizi wa kazi zao.
Abigail anapata shavu kubwa kutoka kwa wasanii wenzake na kutokana na kipaji chake, imefika wakati kuitwa kwenye tuzo kubwa za TMA na Trace.
Siyo kazi ndogo, inaonyesha ni jinsi gani anajituma na anataka mafanikio. Hata hivyo, kwa Tyla amefika tuzo kubwa za Grammy na MTV Base ambazo ni wazi hata Abigail atakuwa anaziota kuwania siku moja.
Ni rahisi tu kama atakaza kwani ana uwezo mkubwa na ameshaanza kutajwa kwenye tuzo kubwa za Afrika.
Hapa tu anamkalisha
Tyla ana uwezo wa kuimba pekee, tofauti na Abigail ni mkali wa kuimba, kucheza, kupiga gitaa, piano na vyombo vingine vya muziki, na ni mojawapo ya mambo yanayompa msanii ramani ya kufikia chati za juu na tuzo kubwa.
Ukimsikiliza Abigail utagundua ana kitu zaidi ya Tyla kuanzia sauti yake na namna ya kutumia ala za muziki ambazo alijifunza tangu akiwa na miaka mitano shuleni.
Kwa kigezo cha kupima ujuzi basi Abigail anapita bila wasiwasi na Tyla akaonekana wa kawaida kwani biashara ya muziki ndiyo inambeba kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji na shoo nyingi anazozipata.
Tatizo uwekezaji
Hapa ndipo Abigail anatakiwa kukaza zaidi kwani nchi kama Nigeria na Afrika Kusini ziko siriazi kuwafanyia promosheni wasanii wao wanaowaamini kwa vipaji hivyo vitaleta manufaa.
Kinachoonekana kwa Tyla ni uwekezaji mkubwa uliowekwa kwenye muziki wake tofauti na Abigail ambaye anapambana mwenyewe kupata platfom kimataifa.
Ni nafasi pia kwa wadau wa muziki wanaokubali uwezo wake zikiwamo produksheni na kampuni za muziki kimataifa kuona ana nini na kumtangaza zaidi kimataifa kama ilivyo kwa Tyla.

Mifano ya wasanii wa Nigeria kama Ayra Starr, Tems ni miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri duniani kutokana na vipaji vyao kuzingatiwa na wawekezaji waliweka pesa ndefu na sasa wanakula matunda ya uwekezaji huo.
Uwezekano wa nyota huyo kupata mwekezaji mzuri wa kimataifa upo na kwani Abigail ameshateka soko la Tanzania na Afrika Mashariki hivyo akipata menejimenti nzuri ya kimataifa uwezo wa kushindana na wasanii wa Nigeria mkubwa kwake.