Abdulla ageukia ripoti ya Tume ya Haki Jinai

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema ripoti ya Tume ya Haki Jinai inadhihirisha kuwa, utendaji wa taasisi hizo nchini hauridhishi kwa kuwa wananchi wameonesha uhitaji wa kufanya mabadiliko katika utoaji wa huduma unaozingatia haki na uwazi.

Amesema mapendekezo hayo yapo ya Muungano na Zanzibar yakijumuisha udhibiti wa makosa ya rushwa, dawa za kulevya, udhibiti wa makosa ya baharini na miundo ya taasisi katika uwajibikaji na uzingatiaji wa misingi ya utawala bora katika kuwahudumia wananchi.

 Abdulla amesema hayo leo Jumapili Februari 2, 2025 katika warsha wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyofanyika Mjini Zanzibar.

 “Dhamira ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kunakuwa na mfumo unaozingatia haki na utawala bora katika utendaji kazi kwa taasisi za haki jinai hasa katika kuwahudumia wananchi,” amesema Abdulla. 

“Hivyo, niwatake wadau wote wanaoguswa katika taasisi hizi kufanya kazi kwa kushirikiana Tanzania bara na Zanzibar kwa kuzingatia maadili, weledi na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yenu ili kudumisha haki.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Mapendekezo  ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohammed Chande Othman amesema tume hiyo imepokea mapendekezo kutoka kwa makundi mbalimbali ikiwamo Jeshi la Polisi lililoshauri kuboreshwa kwa mifumo ya ajira kwa kuangaliwa upya vigezo vya kuajiri.

 Mapendekezo mengine amesema ni kuangaliwa kwa suala la muhali kwa jamii ambalo huchangia kesi nyingi kumalizika nje ya vyombo vya sheria na kutotoa matokeo chanya.

Chande amesema kwa upande wa wananchi, wameomba kuzingatiwa mazingira bora ya upelelezi na ukamataji wenye kuzingatia misingi ya haki na utu, vyombo vya sheria kutenda haki bila ya ubaguzi na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa watendaji wa taasisi za haki jinai watakaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Baadhi ya wadau wa masuala ya haki za binadamu akiwamo Juma Mbaraka wameshauri kuwepo kwa sera ya haki jinai na chombo huru kitakachosimamia watendaji wa taasisi chunguzi pamoja na kufanyiwa mapitio kwa miundo na mifumo ili haki ipatikane kwa wananchi wote na kwa wakati. 

Awali, akiwasilisha mada juu ya kujenga uwelewa wa haki  jinai, mjumbe wa kamati hiyo, Dk Yahya Khamis Hamad amesema ili kufanya kazi kwa kufuata misingi ya haki na sheria ni lazima kuboreshwa kwa sheria na mitalaa ya vyuo vya mafunzo na Jeshi la Polisi.

 “Hali duni ya maisha imekuwa sababu mojawapo inayochangia kutopatikana haki kwa baadhi wa walalamikaji ama walalamikiwa kwa kukosa fursa ya kukata rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa,” amesema Dk Yahya. 

Amesema jambo hilo linahitaji kuangaliwa kwa upeo zaidi kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuwa na Tanzania yenye haki na uwajibikaji kwa kila mwananchi.