A to Z Zugo aeleza pambano lake Ubelgiji lilivyoyeyuka

Abdul Kessy Kasongo maarufu zaidi kwa jina la Abdul Zugo ni mtoto wa Dar es Salaam lakini heshima yake katika mchezo wa ngumi ameenda kuipata Tabora kutokana na mchango wake na namna anavyoupa heshima mkoa huo kupitia mikono yake.

Huenda Abdul Zugo akawa siyo maarufu katika upande wa ngumi lakini tayari yupo kaka yake Seleman Zugo aliyeacha alama kwenye mchezo huo. Kabla ya kuibuka Seleman, alikuwepo Abeid Zugo anayeendelea kupigana hadi sasa.

Kifupi, Zugo anatoka kwenye familia ya mchezo wa ngumi kutokana na mama yake ambaye ni Zena Kipingu, mke wa Kanali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na mkuu wa zamani wa Shule ya Makongo Sekondari, Idd Kipingu, kuwa bondia wa zamani huku kwa sasa akiwa promota wa mchezo huo.

Bondia huyo anaeleza katika watoto wa mama Zugo waliochagua mchezo wa ngumi kama sehemu ya ajira yao ni yeye pekee ndiye amebahatika kupata nafasi ya kucheza ngumi za ridhaa kabla ya kuingia katika ngumi za kulipwa.

Abdul Zugo anashikilia mkanda wa ubingwa wa mabara wa PST na ubingwa wa UBO, akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 15, amefanikiwa kushinda 12 kati ya hayo 10 ni kwa Knockout, amepigwa kwenye pambano moja kwa Technical Knockout ya raundi ya nne wikiendi iliyopita nchini Ghana.

Bondia huyo anayepigana kwenye uzani wa light, amefikia hadhi ya nyota mbili akiwa bondia wa 261 duniani katika mabondia 2635 huku nchini akiwa bondia wa tatu kati ya mabondia 86 wa uzani wake.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Zugo anasema: “Unajua mchezo wa ngumi nimeanza kujifunza nikiwa bado mdogo kwa sababu tayari katika familia yetu alikuwepo kaka yangu Seleman Zugo akicheza.

“Sasa nilikuwa namwona kila siku anapokuwa akifanya mazoezi, mchezo ukanivutia, kama haitoshi kaka yangu mwingine Abeid Zugo naye akawa ananifanya niwafuate kwenye ngumi, hata mama yetu hakuna asiyemjua kupitia ngumi.

“Lakini hata wazazi wangu ni watu wa michezo hivyo ilichangia kusoma katika shule ya michezo, nilisoma Jamiya Nulyia, ipo Mbezi Beach baadaye nikahamia Al-Haramain, shule za dini lakini za michezo.

“Nikawa nasoma huku nikipewa nafasi kubwa ya kushiriki michezo na baada ya kumaliza shule ndiyo nikaweka mizizi katika mchezo wa ngumi za kulipwa kutokana na kaka yangu kunisihi nicheze ngumi.

“Wakati nimeingia kwenye ngumi za kulipwa kutoka ridhaa, nilikutana na bondia mmoja anaitwa Hassan Mandula, alikuwa ni mwanajeshi, ameenda kushiriki hadi michuano ya Jumuiya ya Madola nchini Uingereza.

“Nakumbuka wakati nakutana naye mwaka 2013 nilikuwa na mapambano matatu, tulicheza raundi nane halafu tukatoka sare, hapo mwenzangu alikuwa na uzoefu mkubwa lakini hakuweza kunipiga zaidi ya kutoka sare.

“Kiukweli baada ya pambano hilo ndiyo watu wengi waliweza kunifahamu kutokana na kufanikiwa kuonyesha kiwango kikubwa lakini ikafanya nijihisi naweza kufanya mambo makubwa kwenye ngumi.

“Upande mwingine nilicheza mapambano mengine mawili, nikapotea kabisa kwenye ngumi kutokana muamko wa masuala ya dini.

“Unajua nilikuwa nasoma masomo ya dini sana halafu ngumi ni mchezo wa kupigana kiasi nikawa naona kama haramu hivi yaani kitu ambacho nikifanya napata dhambi.

“Mchezo wa ngumi kwa watu wenye dini unakuwa kama unatia shaka fulani hivi, ikanifanya nikae muda mrefu bila ya kupigana lakini baada ya kuoa niliamua kurejea baada kugundua hii biashara na kazi kwangu.

“Kiukweli nilikuja kubaini naweza kucheza hadi Ulaya baada ya kuamua kurejea ulingoni kutokana na mambo ya kimaisha wakati huo kwenye rekodi yangu inasoma nyota mbili.

Nini kilitokea Ghana wikiendi iliyopita?

“Kwanza nilijiandaa kwenda kupigana na kweli katika hilo niliweza kufanikiwa, nilicheza mchezo mzuri ambao ulimvutia kila mtu katika pambano lile la mkanda wa Ubingwa wa WBO Afrika.

“Lakini changamoto ilikuwa upande wa mwamuzi, muda mwingi alitumia kumlinda bondia wao Faisal Abubakar kabla ya mimi kumueleza msaidizi wangu kwenye kona kuwa mkono umeshtuka.

“Kilichonishangaza mwamuzi akakimbilia kumaliza pambano ikiwa bado nina uwezo wa kuendelea ingawa nilielewa alifanya vile kwa lengo la kumbeba bondia wao.

Kitu gani kimekuwa tofauti ridhaa na ngumi za kulipwa?

“Utofauti niliouna kwenye ngumi za ridhaa, sikupata mafanikio yoyote kwa sababu ni za kujitolea lakini upande wa ngumi za kulipwa ni biashara ambayo naweza kucheza muda wowote nikalipwa fedha.

Kitu gani ambacho huwezi kukisahau kwenye ngumi?

“Nakumbuka kuna kipindi nilienda kupigana Leaders Club bahati mbaya nikakosa mpinzani ila wakati huo kuna bondia alikuwa anataka kupigana na mimi.

“Ikabidi tupime ili kesho yake tupigane, kweli tulipima na siku ya pili tulipanda ulingoni na katika kupigana nilimtungua ngumi mbaya jamaa akawa ameanguka kama mtu mwenye kifafa.

“Lakini baada ya wiki moja nilipewa taarifa amefariki dunia tena akiwa hospitali, iliniumiza sana na ndiyo kitu kilichonifanya nikaingia sana kwenye dini na mchezo nikaachana nao wakati huo.

“Nadhani haina haja ya kuweka majina yake hadharani lakini tulipigana zamani kwenye miaka ya 2015, hali hiyo ndiyo imenifanya nicheze ngumi kama mchezo na siyo uadui.

Ulishakutana na mambo ya ushirikina kwenye ngumi?

“Nakumbuka yalishanikuta japokuwa sikuamini sana, nilichukulia kama Mungu amenikadiria kwa sababu hakuna madhara ya kishirikina yanayomkuta mtu isipokuwa Mungu ametaka yamkute maana Mungu ana uwezo wa kukinga kama unamuamini.

“Kilichotokea, nakumbuka ilikuwa katika pambano ambalo Francis Cheka alicheza pambano kuu, naomba nisimtaje jina huyo bondia niliyecheza naye kwa sababu bado anapigana.

“Nakumbuka imefika raundi ya nne mikono siwezi kurusha, haifunguki kabisa lakini nashukuru Mungu ilimalizika kwa sare kwa sababu nilijitahidi kiasi fulani kukusanya pointi.

Kitu gani kimekutokea hukutarajia?

“Wakati fulani nilipata pambano la kwenda kupigana Ubelgiji, nilishajiandaa kila kitu siku moja kabla ya safari wakati huo hadi tiketi ya ndege na viza nishapata.

“Usiku wake niliamka kumuomba Mungu juu ya safari yangu asubuhi nikaenda kununua vifaa vya kusafiri navyo, nilipoangalia kwenye rekodi nikaona jina langu limeondolewa amewekwa mpinzani mwingine kutoka Venezuela badala yangu kutoka Tanzania.

Una lipi la kuwaambia TPBRC

“Kikubwa ni wao kuendelea kutushika mkono kwa sababu wanayo nafasi kubwa ya kutusaidia mabondia kupata wadhamini ambao wataweza kutusaidia kufikia malengo makubwa maana mchezo wa ngumi unahitaji uwekezaji mkubwa na mabondia wengi tunatoka kwenye maeneo duni.

Kwa nini umekuwa maarufu Tabora?

“Ndiyo sehemu ambayo nimeweka maisha yangu, nashukuru heshima kubwa ambayo mkoa imekuwa ikinipa na nimekuwa nikifanya vizuri kwenye mapambano yangu na wamekuwa wakiandaa hadi mapokezi kwa ajili yangu.

“Unajua Dar es Salaam mabondia wapo wengi, hivyo inakuwa siyo jambo rahisi kukubalika na wote lakini kwa upande wa Tabora, nimekuwa bondia wa mkoa na wanapenda sana kuona napigana ndani ya Tabora.

“Namshukuru sana mama yangu mlezi kwa Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Mkoa Baltida Buruhani ambaye amekuwa chachu japo kwa sasa amehamishwa lakini amenikabidhi kwenye mikono salama kwa aliyekuja sasa. Kikubwa ni kwamba nitaendelea kuiwakilisha Tabora yangu wakati wote nitakapokuwa ulingoni,” anasema Abdul Zugo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *