Bilionea Ratcliffe kwenye mpango wa kuirudisha Man United juu – Sehemu ya tano

Erick ten Hag ana bahati kuendelea kuwa kocha wa Manchester United.

Makocha tisa walifikiriwa na Man United kabla ya kuchukua uamuzi wa kubaki na Ten Hag.

Hiyo ina maana, Ten Hag alijiweka kwenye hatari ya kufutwa kazi. Bosi mpya, tajiri Sir Jim Ratcliffe, ambaye ni shabiki mnazi wa Man United hakuwa akipendezwa na namna timu ilivyokuwa ikicheza msimu uliopita.

Alihisi kocha ni tatizo na hapo ikaelezwa kuwekwa ubaoni majina ya makocha tisa kwenye orodha yao; Gareth Southgate, Kieran McKenna, Roberto De Zerbi, Thomas Frank, Marco Silva, Mauricio Pochettino, Thomas Tuchel, Ruben Amorim na Roberto Martinez.

Baada ya kumkosa mtu sahihi, bilionea Ratcliffe aliamua kumbakiza Ten Hag kwenye benchi la ufundi. Lakini, hilo lilibeba ujumbe wa wazi kwamba kibarua cha Mdachi huyo hakipo salama kwa asilimia 100. Mashabiki wanaamini Man United imefanya uamuzi sahihi wa kumvumilia kocha, lakini shida inakuja sehemu moja, tu, Ten Hag sio mtu sahihi wa kumvumilia. Mashabiki wa Man United wanasema Ten Hag kwamba hakuwa na nidhamu wakati anatua England, alipochimba mkwara kwamba Pep Guardiola na Jurgen Klopp zama zao zimefika mwisho. Ten Hag alionekana kuwakosea nidhamu makocha hao, ambapo wote wana rekodi moto kabisa za kubeba mataji makubwa ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya na ndiyo maana walichokuwa wakifanya ni kumwaadhibu kwa kumfunga nyingi uwanjani.

Katika kuweka mipango mizuri Old Trafford, tajiri Ratcliffe amekuja na mabadiliko matano kwenye kikosi hicho linapokuja suala la usajili.

1. Umri mkubwa wa mchezaji mpya anayesajiliwa ni miaka 25

2. Hakuna kusajili wachezaji wenye majina makubwa (masupastaa)

3. Staili ya uchezaji inaamuliwa na mkurugenzi wa ufundi ambaye ni Jason Wilcox

4. Kocha atasema tu anataka mchezaji wa nafasi gani na si kutaja jina la mchezaji

5. Kampuni yake ya Ineos itamtumia kocha majina matatu ya kila nafasi anazotaka anachague mmoja wa kusajiliwa.

Hiyo ndiyo dira mpya ya Man United ya bilionea Ratcliffe katika harakati zake za kuhakikisha kikosi hicho hakifanyi matumizi ya pesa kizembe, huku ikijaribu kuunda wachezaji ambao watakuwa na tija kwenye timu.

Bilionea Ratcliffe ana shughuli pevu kwenye kuirudisha timu hiyo katika makali yake. Ametengeneza mpango wa kwanza wa miaka mitatu, kuhakikisha Man United inakuwa na uwezo wa kubeba ubingwa itakapofika 2028. Kocha wa zamani wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson anaamini bilionea huyo Mwingereza atafanikiwa kwenye jitihada zake za kumaliza kama si kuondoa kabisa pengo la ubora lililopo baina ya timu hiyo na Manchester City na Liverpool.Kwenye mpango wa miaka mitatu kwa maana ya malengo ya ubingwa ya mwaka 2028, Ten Hag ana msimu huu wa kuonyesha kitu anachoweza kufanya. Akishindwa kufanya hilo, itakuwa ngumu kumwona akiendelea kubaki kwenye kikosi hicho zaidi ya 2025.

Ratcliffe anafahamu wazi ana ahadi aliyowapa mashabiki wakati anachukua timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford. Bosi huyo ni shabiki, hivyo kama mambo hayaendi vizuri, hata yeye anakosa furaha. Kilio cha mashabiki ni kilio chake pia tajiri.

Ten Hag ana bahati kuaminiwa kwenye kipindi hiki, tofauti na watangulizi wake David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer – ambao walikuwa kwenye kipindi cha mabosi wasiojali soka wala wasio na ushabiki wa timu hiyo na bado walifunguliwa milango ya kutokea mapema kabisa.

Bilionea si mtu wa kuchukua muda mrefu kujivua gamba. Akiona mambo yake yanashindwa kwenda kama anavyotaka, haoni shida kwake kufanya mabadiliko. Na jambo hilo linaweza kuwa kwenye benchi la ufundi hadi kwa wachezaji ndani ya uwanja. Kwa namna hiyo, wachezaji kama Antony, Casemiro, Andre Onana na Mason Mount wanapaswa kujitazama sana, kwa sababu walisajiliwa kwa pesa nyingi, hivyo wanapaswa kutoa huduma kulingana na pesa iliyolipwa kuwasajili.

Usajili wa wachezaji wapya kwenye timu kwa sasa unaangaliwa sana na ishu ya Financial Fair Play, hivyo mchezaji hapaswi kuwa mzigo kwenye timu, anatakiwa atoe huduma kulingana na pesa iliyolipwa kwa sababu si wakati wote ataletwa mchezaji mwingine wa kuja kufanya kile alichoshindwa kufanya.

Kwa jambo hilo ndiyo maana tajiri Ratcliffe amekwenda Man City kwenda kuwachukua watu kama Omar Berrada – ambao watakuwa na majukumu kwenye kufanya usajili, kuleta watu watakaokuwa sahihi. Dan Ashworth amechukuliwa kutoka Newcastle United kuja kuwa mkurugenzi wa soka.

Bosi huyo amefanya maboresho muhimu kwenye idara hiyo ya uongozi wa juu ili kuhakikisha mipango yote inakuwa chini ya watu sahihi. Baada ya hapo, tajiri huyo ameweka wazi juu ya mpango wa kuujenga upya Uwanja wa Old Trafford na miundombinu ya kwenye viwanja vya mazoezi huko Carrington.

Maboresho kwenye viwanja vya mazoezi Carrington yamekwenda vizuri na sasa kipaumbele kipo kwenye kuujenga upya Uwanja wa Old Trafford. Uwanja huo ulionekana kuchakaa na hilo ndilo linamfanya Ratcliffe kuamini linachangia kuifanya Man United kuwa timu ya kawaida.

Uwezo wa Old Trafford ya sasa ni kuingiza watazamaji 74,310 wanaoketi, lakini mchoro mpya wa uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 100,000. Ratcliffe anaamini mazingira mazuri ya uwanja yanakuwa kivutio kwa wachezaji wengi kutaka kuja kujiunga na timu hiyo, huku malengo makubwa ni kuifanya Old Trafford si tu kuwa na uwanja wa soka, bali sehemu ya kivutio cha utalii na klabu kuvuna pesa kwenye mpango huo.

Old Trafford mpya pia itakuwa na maduka na hoteli za kisasa kuchangia mapato kwenye timu, huku kinachoelezwa ujenzi wake unaweza kugharimu zaidi ya Pauni 2 bilioni. Tajiri huyo anaamini asilimia 27.7 ya hisa, ambazo zinaweza kupanda, huku majukumu yake makubwa yanakuwa kwenye mambo ya soka.

Wamiliki wakuu wa klabu hiyo, familia ya Glazer yenyewe itakuwa inajishughulisha na mambo mengine, huku Ratcliffe akisimamia eneo muhimu zaidi linalofanya uhai wa timu hiyo katika kujikusanyia mashabiki, eneo la soka.

Moyo wake wa kutokupenda kushindwa ndicho kitu kinachowapa matumaini wengi kwamba ataifanya Man United kuwa timu tishio. Ratcliffe anavutiwa na namna Man City ilivyopambana kutoka chini na sasa inachuana na vigogo kama Real Madrid, timu ambazo kwa sasa ukiziweka kucheza na Man United inakuwa kama bondia wa uzito wa juu dhidi ya bondia wa uzito wa unyoya. Bilionea huyo anaamini Man City imefikia hapo kwa kuweka watu sahihi kwenye maeneo sahihi, ambao walitoa pesa kusajili wachezaji kwa kuzingatia vipaji. Anavutiwa na utendaji wa kocha Pep Guardiola, ambaye hahitaji mchezaji mwenye jina kubwa kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja. Kwa mfano huyo ndiyo maana amefuta ishu ya kusajili Galacticos huko Old Trafford. Wachezaji kama Paul Pogba, Ronaldo, Neymar, Karim Benzema hawana nafasi tena.