Maagizo ya Rais Samia kwa Bashe, Aweso

Peramiho. Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kufuatilia taarifa za uwepo wa wakulima wa kahawa wanaokatwa kinyemela sehemu ya fedha za mauzo ya zao hilo.

Hatua ya kukatwa kwa fedha hizo, inatokana na kilichoelezwa na Rais Samia kuwa, bei ya kahawa mwaka huu imeongezeka maradufu, hivyo baadhi ya vyama vya ushirika vinatumia hiyo kama fursa ya kuwadhulumu wakulima.

Hata hivyo, mmoja wa wakulima wa zao hilo, amesema wanakatwa fedha hizo pale malipo ya mauzo yao yanapopitia katika vyama hivyo.

Sambamba na hilo, mkuu huyo wa nchi pia alimwelekeza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha mradi wa maji Mtyangimbole unakamilika kufikia Desemba mwaka huu.

Msingi wa maelekezo yake hayo ni kile alichofafanua kuwa jana ameweka jiwe la msingi katika mradi huo, hakuna sababu ya kusubiri zaidi ya wananchi kuona maji yanatoka.

Rais Samia ameyasema hayo kwa nyakati tofauti leo Jumanne Septemba 24, 2024 akiwa katika shughuli mbalimbali ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita mkoani Ruvuma.

Agizo kwa Bashe

Rais Samia amemtaka Waziri Bashe kuhakikisha anafuatilia malalamiko ya wakulima wa kahawa kukatwa sehemu ya fedha zao za mauzo na vyama vikuu vya ushirika.

Msingi wa maelekezo yake hayo ni malalamiko ya wakulima wa zao hilo, waliosema kuna tabia ya baadhi ya vyama vikuu vya ushirika kuwakata fedha zao.

Rais Samia Suluhu Hassan akimweleza jambo Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhi nafaka mkoani Ruvuma katika hafla iliyofanyika katika eneo la Luhimba wilayani Madaba, leo Septemba 24, 2024. Picha na Edwin Mjwahuzi

Hilo linathibitishwa na Anthon Tembo, anayelima kahawa mkoani Ruvuma, akisema fedha hizo zinakatwa kabla hazijafika kwa mkulima.

“Tukishauza fedha zinapelekwa kwenye chama kwa ajili ya kutugawia. Kwa sasa gunia la kahawa ni Sh412,000 kwenye kiasi hicho wanakamata hadi Sh30,000” amesema mkulima huyo.

Hata hivyo, amesema makato hayo si stahiki kwa vyama hivyo, badala yake kinachofanywa ni dhuluma inayosababishwa na tamaa ya wachache.

Katika maagizo yake hayo, Rais Samia amesema: “Ninatambua uwepo wa malalamiko ya wananchi kwamba kwa sababu kahawa imepanda bei, baadhi ya vyama vikuu vya ushirika (hakuvitaja) vinawakata wakulima kinyemela.”

Amemtaka Bashe kufuatilia ili kuwa na mfumo wa wazi utakaowafanya wakulima kuona wanachouza na uhalisia wa makato yao.

“Huu ujanja ujanja unaoendelea unapaswa kukomeshwa,” amesema mkuu huyo wa nchi alipozungumza na wafanyakazi wa shamba la Aviv Limited lenye ukubwa wa hekta 200.

Hata hivyo, amesema ongezeko la bei hiyo na malipo ya haraka kwa wakulima wa kahawa ni matokeo ya juhudi za Serikali za kuongeza ufanisi katika mauzo ya zao hilo.

Kadhalika, Rais Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kujipanga vema na masharti yanayotolewa na masoko ya kimataifa ya kahawa, hasa lile la uzalishaji bila kukata misitu.

Pamoja na kutokata misitu, amesema masharti mengine ni kukagua, kuyasajili na kupeleka taarifa za mashamba kwenye masoko hayo, ili ijulikane linakotoka zao husika.

“Wanatambua tusikate misitu, kweli kwao wameshakata lakini sisi tunataka soko, tunapaswa kuhakikisha tunayatimiza masharti ili kupata soko,” amesema.

Amewataka wakulima watumie fursa ya uwepo wa bei kubwa ya kahawa mwaka huu kuhifadhi fedha, ili wasitaabike katika nyakati ambazo bei ya zao hilo itashuka.

“Misimu ikiwa mizuri na bei ikiwa nzuri tuwe na mifumo ya kujiwekea akiba, ili mabadiliko ya tabianchi yanapotokea tuwe na akiba,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameutaka uongozi wa shamba hilo, unafanye shughuli za kijamii ujikite katika uchimbaji wa visima vya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima.

Amesema kufanya hivyo kutawawezesha wakulima kuzalisha kahawa kwa umwagiliaji na kuuza kwa Aviv.

Kwa upande wake, Waziri Bashe amesema shamba hilo ni moja kati ya 50 yanayozalisha kahawa na kwamba hilo ni kubwa zaidi ya mengine yote.

Amesema asilimia 60 ya kahawa inayozalishwa na shamba hilo inauzwa nje ya nchi kwa Kampuni ya Strabag.

Hata hivyo, amesema wastani wa bei ya kahawa mwaka huu ni Dola 4.3 za Marekani, kiwango ambacho ni tofauti na nyakati zilizopita.

Agizo kwa Aweso

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha mradi wa maji wa Mtyangimbole unakamilika baada ya miezi mitatu.

Ametoa agizo hilo muda mchache baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo, ukiwakilisha miradi mingine 30 ya maji mkoani Ruvuma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la Msingi la mradi wa maji wa Mtyangimbole, Madaba mkoani Ruvuma leo Septemba 24, 2024.

Amesema kwa sababu uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi huo kunaibua matumaini ya wananchi, ni vema kuhakikisha maji yanapatikana haraka.

“Hakikisheni kufikia Desemba mwaka huu maji yanatoka hapa, wananchi wale Krismasi huku wanaoga kwa sababu tumeweka jiwe la msingi tumewapa matumaini,” amesema.

Hata hivyo, amesema matarajio yake kufikia mwakani Serikali chini yake itahakikisha upatikanaji wa huduma ya maji unafika asilimia 85 kwa vijijini na zaidi ya 90 kwa mijini.

Utekelezaji wa hilo, amesema ni kuakisi maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25.

Amewasihi wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji, ili kulinda uhai wake.

Awali, akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa maji, Aweso amesema hadi sasa upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 79, huku mijini ikiwa asilimia takribani 90.

Kwa kuwa kuna miradi inayoendelea kutekelezwa, amesema itakapokamilika, vijijini upatikanaji wa huduma hiyo utafikia asilimia zaidi ya 85 na mjini zaidi ya 90.

‘Kila anayestahili fidia atalipwa’

Kadhalika, Rais Samia amesema hakuna mwananchi atakayeguswa na mradi unaotekelezwa na Serikali asilipwe fidia.

Ingawa inaweza kuchelewa, amesema Serikali itahakikisha inampa kila mwananchi haki yake anayoistahiki.

Rais Samia ametoa hakikisho hilo la fidia kwa wananchi, wakati akijibu ombi la Mbunge wa Madaba, Dk Joseph Mhagama aliyeomba wananchi watakaopitiwa na ujenzi wa barabara ya Makambako walipwe fidia.

“Hakuna mradi utakaopita kwa wananchi, Serikali ichukue ardhi bila kulipa fidia za watu. Inaweza ikachelewa lakini sio kwamba Serikali itaacha kabisa kulipa fidia,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo, amesisitiza uzalishaji zaidi kupitia shughuli mbalimbali kikiwemo kilimo, ili kuijengea uwezo Serikali wa kutekeleza miradi mingi kwa fedha zake za ndani na hivyo kulipa fidia haraka.

“Lakini niwahakikishie hakuna mwananchi atakayedhulumiwa, kila mmoja atakayepitiwa na mradi atalipwa fidia yake,” amesema.

Ammwagia sifa Jenista

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemmwagia sifa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama akimwita kiraka katika utendaji.

“Nalishukuru tumbo lililomtela Jenista Mhagama, mimi pamoja na kwamba ni Rais, lakini namwita kiraka changu. Nikiona mambo huku yameharibika nampeleka na niwahakikishie hakuwahi kukosea,” amesema.

Ujumbe kwa wanaoandamana

Katika hotuba yake alipozungumza na wananchi wa Peramiho, Rais Samia amewataka wananchi wasifikirie kuandamana, badala yake watunze amani.

“Mnawasikia wengine tuandamane, tukapigane hilo sisi hapana, hiyo sio sera yetu. Sisi sera yetu ni kuwa na amani na utulivu, hayo mengine waachieni wenyewe,” amesema.

Rais Samia ameijenga hoja hiyo alipowahamamisha wananchi kujitokeza kupiga kura wakati wa uchaguzi wa serikali za mtaa, akiwasisitiza wawachague viongozi stahiki.