Wafahamu viongozi watano wa Afrika waliong’ang’ania madarakani

Je, unajua kuna viongozi wa Afrika wako madarakani kwa zaidi ya miaka 40 sasa? Na hawana mpango wa kuondoka kwa njia yoyote hasa ya kidemokrasia kama katiba zao zinavyoelekeza.

Viongozi wa mataifa haya wamekuwa wakiandaa uchaguzi na kila muhula wanashinda chaguzi hizo hata kwa njia za udanganyifu au kutumia vyombo vya dola kuwabakisha madarakani.

Mataifa matano ya Afrika yameweka rekodi ya kipekee viongozi wao kukaa madarakani kwa muda mrefu, jambo linalotajwa kukandamiza demokrasia katika mataifa hayo na kuwaacha wananchi katika hali ya umasikini.

Mwananchi inakuletea orodha ya viongozi watano wa Afrika waliokaa madarakani kwa muda mrefu na mambo yaliyowasaidia kubakia madarakani kwa kipindi kirefu bila upinzani mkali kutoka kwa vyama vingine.

Teodoro Obiang Nguema

Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema (82) ndiyo kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi Afrika, amefikisha miaka 45 sasa tangu alipoingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi, Agosti 3, 1979.

Nguema ni Rais wa pili wa Equatorial Guinea tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Waspaniola, mwaka 1968. Alimpindua mjomba yake, Francisco Macías Nguema ambaye utawala wake ulitawaliwa na ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mwaka 1987, Nguema alianzisha chama cha siasa cha PDGE ambacho hadi mwaka 1991 kilikuwa chama pekee nchini humo, kikiongoza Serikali. Mwaka 1989, alishinda uchaguzi kwa kupita bila kupingwa na pia amekuwa akishinda katika chaguzi zote zilizofuata.

Utawala wake ulifanya mabadiliko ya katiba mara kadhaa ikiwamo ya mwaka 2011 yaliyoweka ukomo wa muda wa kuwa madarakani ambao ni vipindi viwili, hata hivyo kifungu hicho hakitumika katika utawala wake. Pia, aliondoa ukomo wa umri wa mgombea urais.

Mwaka 2012, kiongozi huyo alimteua mtoto wake, Teodoro Nguema Obiang Mangue kuwa Makamu wa Rais, jambo lililodhaniwa ilikuwa kumuandaa mwanaye kushika madaraka, lakini hadi sasa bado ni Rais na mwanaye ni Makamu wa Rais.

Paul Biya (91) ni Rais wa Cameroon anayeliongoza Taifa hilo la Afrika Magharibi akitumia kundi dogo la wasaidizi wake anaowateua na wanaomsaliti, amekuwa akiwaadhibu kwa kuwatimua nchini mwake.

Biya aliingia madarakani Novemba 6, 1982, akiwa ni Rais wa pili wa Cameroon baada ya Ahmadou Ahidjo. Kabla ya kushika nafasi hiyo, Biya alikuwa Waziri Mkuu wa Cameroon, nafasi ambayo ameitumikia kuanzia mwaka 1975 hadi 1982.

Ni mwiko katika Taifa hilo kuzungumzia kuhusu kuachiana madaraka, hata kwa watu wake wa karibu. Ameweka rekodi ya kuwa Rais mwenye umri mkubwa duniani aliye madarakani na anashika nafasi ya pili kwa kukaa madarakani kwa miaka 42.

Katika uchaguzi wa mwaka 2018, Biya alikabiliwa na ushindani mkubwa katika historia ya uongozi wake, hata hivyo alitangazwa mshindi kwenye uchaguzi huo uliotawaliwa na vitendo vya ukatili hasa kwa wapinzani.

Denis Sassou Nguesso

Kiongozi anayeshika nafasi ya tatu kwa kukaa madarakani muda mrefu ni Rais wa Jamhuri ya Congo (Brazzaville), Denis Sassou Nguesso (80) ambaye mwaka huu ametimiza miaka 40 tangu alipotwaa madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 1979.

Tofauti na viongozi wengine waliotawala mfululizo, Nguesso alikuwa Rais wa Congo kwa miaka 13 kuanzia mwaka 1979 hadi 1992. Baadaye alirejea tena madarakani mwaka 1997 hadi mwaka huu amefikisha jumla ya miaka 40 akiwa Rais wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Alichaguliwa mwaka 2016 baada ya kupitishwa kwa katiba mpya na baada ya hapo amekuwa akichaguliwa kwenye chaguzi zinazofanyika na mwaka 2022 alichaguliwa kwa muhula wa nne kuwa kiongozi wa Taifa hilo.

Rais Nguesso amekuwa akikosolewa kwa ubadhirifu wa fedha hasa kwa misafara yake. Mwaka 2005, Rais Nguesso alikoselewa kwa  kwenda Marekani na watu wake 50 walikokaa siku nane kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) kwa dakika 15 tu.

Gazeti la Sunday Times liliripoti kwamba, ziara hiyo iligharimu Dola 295,000 za Marekani na maelfu mengine ya dola yalitumika kugharamia vyumba walivyolala huko Mnahattan, New York, Marekani.

Yoweri Museveni

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni (80) ndiyo amekaa madarakani kwa muda mrefu, mwaka huu amefikisha miaka 38 huku akitarajiwa kugombea muhula mwingine katika uchaguzi ujao wa mwaka 2026.

Museveni aliingia madarakani mwaka 1986 kwa njia ya mapinduzi kupitia kundi la waasi la NRM ambalo baada ya mapinduzi hayo likawa chama tawala ambacho kimekuwa madarakani tangu wakati huo hadi sasa.

Amefanya mabadiliko ya katiba kumruhusu aendelee kuwepo madarakani na moja ya mambo yaliyobadilishwa ni kuondoa ukomo wa umri wa kuwa madarakani pamoja na kuongezwa muda wa muhula kutoka miaka mitano hadi saba.

Wiki iliyopita, mtoto wa Museveni, Muhoozi Kainerugaba, aliyekuwa anatajwa kurithi kiti cha urais kutoka kwa baba yake, alitangaza kumpendekeza baba yake kwenye nafasi ya urais na yeye atabaki kutumikia nafasi yake ya Ukuu wa Majeshi ya Uganda (CDF).

Mfalme Mswati III

Nafasi ya tano ya viongozi waliotawala kwa muda mrefu, ni Mfalme Mswati III (56) wa Eswatini (zamani Swaziland) ambaye amefikisha miaka 38 kama mfalme wa taifa hilo dogo linalopatikana Kusini mwa Afrika.

Mswati III alitawazwa kuwa mfalme Aprili 25, 1986 akiwa na umri wa miaka 18 tu. Alikuwa ni mtoto wa Mfalme Sobhuza II na mke wake mdogo, Ntfombi Tfwala. Wakati huo, Mswati III aliweka rekodi duniani ya kuwa kiongozi mdogo wa kitaifa.

Tofauti na mataifa mengine ya Afrika yanayofuata mfumo wa kidemokrasia, Eswatini inafuata mfumo wa kifalme unaorithishwa kwa watu walio katika ukoo wa kifalme na siyo kwa kugombea na kuchaguliwa.

Mswati III kama mkuu wa nchi, anakosolewa kwa kukumbatia utamaduni wa kuoa wake wengi, jambo linaloongeza gharama na mzigo kwa Serikali huku wananchi wake wakiendelea kuwa masikini, wakikosa huduma muhimu za kijamii.