
Mkuu wa Majeshi wa Iran Jenerali Mohammed Bagheri ameuawa katika shambulizi la Israeli, televisheni ya taifa ya Iran imeripoti leo Ijumaa. “Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Jeshi, ameuawa shahidi,” televisheni hiyo imesema.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kamanda Mkuu wa Walinzi wa Mapinduzi Jenerali Hossein Salami, ameuawa katika shambulio la Israeli, mashirika ya habari ya Iran Tasnim na Mehr yameripoti, huku televisheni ya taifa ikiripoti kuwa makao makuu ya kikosi hicho yameteketea kwa moto na moshi ukifuka kutoka kwenye jengo hilo lililoko mtaa wa Pirouzi mashariki mwa Tehran. Mkuu wa majeshi ya Iran Mohammed Bagheri pia ameuawa katika shambulio hilo, televisheni ya taifa imesema.
Jeshi la Israeli limeripoti kuwa ndege zake za kivita zinaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi na nyuklia vya Iran.
“Marubani wetu wameshambulia na wanaendelea kushambulia maeneo ya kijeshi na malengo zinazohusiana na mpango wa nyuklia katika maeneo mbalimbali ya Iran,” amesema msemaji wa jeshi la Israeli Brigedia Jenerali Effie Defrin.
Wanajeshi wa Israel wajaribu kuzuia takriban ndege 100 zisizo na rubani zilizorushwa na Iran
Vikosi vya Israeli vinajaribu kuzuia takriban ndege 100 zisizo na rubani zilizorushwa na Iran kujibu mashambulizi ya Israeli, msemaji wa jeshi la Israel amesema siku ya Ijumaa asubuhi. “Iran imezindua takriban ndege 100 zisizo na rubani kuelekea eneo la Israel, na tunajaribu kuzizuia,” Brigedia Jenerali Effi Defrin amesema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni mwendo wa saa 2:00 asubuhi (1:00 saa za Ufaransa).
Saudi Arabia inalaani “uchokozi wa Israeli” dhidi ya Iran
Saudi Arabia imelaani mashambulizi mabaya ya Israeli dhidi ya Iran siku ya Ijumaa, na kuyataja kuwa “uchokozi wa wazi” dhidi ya “nchi ndugu.” Ufalme huo “unaonyesha kulaani vikali na kukemea uchokozi wa wazi wa Israeli dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi ndugu, ambayo inadhoofisha mamlaka na usalama wake na ni ukiukaji wa wazi wa sheria na kanuni za kimataifa,” Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia imesema katika taarifa yake.
Donald Trump aiambia Fox News kuwa alifahamishwa kuhusu shambulio hilo
Rais wa Marekani Donald Trump ameiambia Fox News kuwa alifahamu kuwa Israeli itaendesha mashambulizi nchini Iran na akatangaza kwamba Tehran haipaswi kupata silaha za nyuklia. “Iran haiwezi kuwa na bomu la nyuklia, na tunatumai kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Tutaona,” Bw. Trump amesema, akinukuliwa na mtandao wa televisheni wa Marekani siku ya Ijumaa. Mazungumzo kati ya Washington na Tehran yamepangwa kuanza siku ya Jumapili nchini Oman.
Takriban watu 50, wakiwemo wanawake na watoto, wamejeruhiwa katika shambulio hilo
Takriban watu 50, wakiwemo wanawake na watoto, wamejeruhiwa katika shambulio hilo, kulingana na televisheni ya taifa. “Kufuatia shambulio la Israeli, takriban watu 50 waliojeruhiwa wamepelekwa katika Hospitali ya Chamran (huko Tehran), ikiwa ni pamoja na angalau wanawake 35 na watoto,” televisheni ya taifa imesema baada ya mashambulizi hayo, ambayo yamelenga maeneo ya nyuklia ya Iran pamoja na majengo ya makazi mjini Tehran.
Wizara ya Mafuta ya Iran yasema viwanda vya kusafisha mafuta na bohari “havikuathiriwa”
Wizara ya Mafuta ya Iran imesema siku ya Ijumaa kuwa vituo vikuu vya kusafisha mafuta na ghala za mafuta nchini humo havikuathiriwa na shambulio baya la Israeli na kwamba operesheni zao zinaendelea. “Hakuna uharibifu wowote uliotokea katika vituo vya kusafisha mafuta na ghala za mafuta nchini, na kwa sasa, shughuli za kuweka vifaa hivi na usambazaji wa mafuta zinaendelea katika mikoa yote ya nchi bila usumbufu,” imesema taarifa ya wizara hiyo.