UN yaishtumu Iran kukiuka wajibu wake wa kinyuklia

Iran imeapa kuendeleza mpango wake wa nyuklia licha ya hatua mpya ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kuishutumu kwa ukiukaji wa wajibu wake wa kinyuklia — na sasa, Tehran imeanzisha ujenzi wa kituo kipya cha kurutubisha urani katika eneo la usalama wa hali ya juu.

Hatua hiyo inakuja baada ya bodi ya magavana wa IAEA mjini Vienna kupitisha azimio linalosema Iran haijatekeleza kikamilifu majukumu yake chini ya Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), na kuchochea hofu ya kurejea kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa ya pamoja, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Shirika lake la Nishati ya Atomiki wamesema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina budi kujibu azimio hili la kisiasa.”

Bodi ya IAEA yagawanyika

Balozi wa Iran katika IAEA, Reza Najafi, alikosoa vikali uamuzi huo, akisema ulikuwa wa kisiasa na kulazimishwa na Marekani pamoja na washirika wake wa Ulaya.

“Leo tunashuhudia kwamba Bodi ya Magavana ya IAEA imegawanyika kabisa, na azimio lililowasilishwa na mataifa ya E3 na Marekani kwa misingi ya kisiasa limepitishwa kwa kura chache sana. Hii ni mara ya pili kwa Bodi ya Magavana kutounga mkono kikamilifu azimio kama hilo.”

Iran Teheran 2025 | Waziri Araghchi akutana na Mkuu wa IAEA Grossi kwa mazungumzo ya nyuklia – 16.04.2025
Iran Teheran 2025 | Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi akikutana na Mkuu wa IAEA Rafael Mariano Grossi kwa mazungumzo ya nyuklia – 16.04.2025Picha: Iranian Foreign Ministry/AP/picture alliance

Katika kura hiyo, mataifa 19 yaliunga mkono azimio hilo, huku Urusi, China na Burkina Faso zikilipinga, na 11 yakijizuia kupiga kura.

IAEA imeeleza kuwa kwa miaka kadhaa sasa, Iran haijafichua kikamilifu shughuli zake za awali za nyuklia. Wachunguzi wake wamegundua chembechembe za urani kwenye maeneo ambayo hayakutangazwa rasmi kuwa vituo vya nyuklia — hali inayoongeza wasiwasi wa kimataifa.

Tehran yajibu kwa kuimarisha uwezo wake

Licha ya madai ya Tehran kwamba mpango wake ni wa amani, Iran inaendelea kurutubisha urani kwa viwango vinavyokaribia kiwango kinachofaa kutengeneza silaha, jambo linalozua tahadhari kwa mataifa ya Magharibi na Israel.

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Behrouz Kamalvandi, amesema kituo hicho cha tatu cha kurutubisha urani tayari kimejengwa katika eneo salama na lisiloweza kushambuliwa.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alisema Iran “haitakubali kutishwa kwa nguvu” na kuonya kuwa hata kama vituo vya nyuklia vya nchi hiyo vitashambuliwa, Iran itavijenga upya.

Akizungumza katika mji wa Ilam, Pezeshkian aliilaumu Marekani na Ulaya kwa kuiwekea Iran vikwazo na mashinikizo ili kudhoofisha maendeleo yake.

“Wanafanya hivi kwa sababu wanadhani (Marekani na Magharibi) kwamba wanaweza kuzuia maendeleo yetu kwa mashinikizo haya,” alisema.

“Si kwamba wakiharibu vituo vyetu kwa mabomu kila kitu kitaisha — uwezo huu upo kwenye fikra zetu, kwa hiyo, chochote watakachofanya, tutajenga tena.”

MAKTABA | Iran | Rais Masoud Pezeshkian akiwa Tehran
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema Tehran “haitasalimu amri kwa nguvu na vitisho vya mataifa ya MagharibiPicha: Iranian Presidency/ZUMA Press Wire/picture alliance

“Tuwe na imani na tumtegemee Mungu, tuna uwezo wa kushinda matatizo yote. Hatujajitolea kwa Marekani na washirika wake. Hii haimaanishi kwamba tunataka kupigana na dunia, tunataka kuzungumza na dunia, lakini hatutakubali kunyanyaswa, kudhulumiwa wala kutishwa.”

Mazungumzo ya nyuklia yatingwa

Mivutano hii inazidi kuathiri mazungumzo yanayoendelea kati ya Washington na Tehran kuhusu mkataba mpya wa nyuklia, ambayo duru ya sita ya mazungumzo imepangwa kufanyika Jumapili hii huko Muscat, Oman.

Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema wiki hii kuwa hana tena matumaini makubwa kuhusu mafanikio ya mazungumzo hayo.

Wakati huo huo, kwa tahadhari, Marekani imeanza kuwaondoa wafanyakazi wake wasio wa lazima nchini Iraq, huku ubalozi wake nchini Israel ukiagiza wafanyakazi wake wabaki ndani ya maeneo salama ya Tel Aviv — ikihofia uwezekano wa mashambulizi ya Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, uamuzi wa IAEA kwamba Iran iko kwenye ukiukaji wa wajibu wake wa nyuklia “utazidi kuyatatiza mazungumzo haya.”

Mataifa ya Ulaya yamesema bado kuna nafasi kwa Iran kushirikiana na IAEA ili kuepusha mzozo mkubwa zaidi. Hata hivyo, iwapo Tehran haitatoa majibu yanayokubalika, suala hilo linaweza kufikishwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa msimu wa kiangazi mwaka huu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia, mjumbe maalum wa Marekani, Brian Witkoff, anatarajiwa kusafiri kwenda Muscat kwa ajili ya duru ya sita ya mazungumzo hayo siku ya Jumapili.

Chanzo: APE, DPAE,AFPTV

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *