Haya yamesemwa Alhamis na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi UNHCR.
Kwa mujibu wa ripoti ya UNHCR ya kila mwaka ya dunia, wakimbizi milioni 1.6 walirudi makwao kutoka mataifa ya kigeni mwaka 2024, hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.
Watu walioachwa bila makao katika mataifa yao pia walirudi katika maeneo waliyokuwa wakiishi.
Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema, mkondo huo uliendelea mapema mwaka 2025 huku kukishuhudiwa ongezeko la Wasyria kurudi nyumbani kufuatia kuangushwa kwa utawala wa dikteta Bashar al-Assad mnamo Disemba 2024.
Kulingana na shirika hilo la wakimbizi, karibu Wasyria milioni 2 wamerudi katika nchi yao iliyokuwa imezongwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Grandi ameelezea suala hili kama ishara ya matumaini.
Kufikia mwishoni mwa Aprili 2025, idadi ya watu walioachwa bila makao duniani ilikuwa ni watu milioni 122, hilo likiwa ongezeko la watu milioni mbili ikilinganishwa na mwaka 2024.
Kati ya hao, asilimia 60 ni wakimbizi wa ndani ya mataifa yao huku thuluthi mbili ya wale waliovuka mipaka wakiwa wanaishi katika nchi jirani.