Bajeti ya Kenya ni zaidi ya shilingi trilioni 4

Hata hivyo shughuli hiyo imeendelea huku bajeti ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki ya mwaka 2025/26 ikikadiriwa kuwa shilingi trilioni 4.26, kiwango kilichoongezeka kutokea shilingi trilioni 3.87 mwaka uliopita wa fedha. 

Sekta ya elimu imetengewa hela nyingi zaidi kwenye bajeti hii mpya nayo kaunti ya Nairobi itavuna shilingi bilioni 21.1 kwenye mgao wa kufanikisha mfumo wa ugatuzi.

Akiwa waziri wa kwanza fedha kutokea kambi ya upinzani,John Mbadi alifungua ukurasa mpya wa usimamizi wa hela za umma katika bajeti mpya ya mwaka 2025/26.

Bajeti ya mwaka huu imeitaka kila wizara,idara na mamlaka kuwasilisha maombi ya pesa na kusadikisha matumizi yake.

Hakuna nyongeza ya kodi wala kodi mpya

Waziri wa fedha wa Kenya John Mbadi alibainisha kuwa mageuzi hayo ni msingi thabiti kwa viongozi watakaomrithi.

“Mswada wa fedha wa 2025 haujapendekeza kodi mpya wala kuongeza kodi. Kutokana na mapendekezo ya mageuzi tunatazamia kuliongeza pato letu kwa shilingi bilioni 30,” alisema Mbadi.

Waziri wa Fedha Kenya akiwa na bajeti ya nchi hiyo
Waziri wa Fedha Kenya akiwa na bajeti ya nchi hiyoPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Pato la serikali linakadiriwa kuwa shilingi trilioni 3.39 na lile la kawaida kufikia shilingi trilioni 2.84 kwasababu ya mageuzi ya kodi yanayoendelea kutekelezwa.

Serikali inapanga pia kutumia shilingi trilioni 3.1 kugharamia mahitaji ya kila siku, shilingi bilioni 725.1 kufadhili miradi ya maendeleo na kuzitengea serikali za kaunti shilingi bilioni 405.1., kiwango ambacho kimeongezeka kwa shilingi bilioni 17.6.

Kaunti ya Nairobi ndiyo itakayopokea mgao mkubwa zaidi wa shilingi bilioni 21.1.

Sekta ya elimu itavuna pakubwa kwa kutengewa shilingi bilioni 701 ijapokuwa bado kiasi hicho hakitakidhi mahitaji yote.

Sekta ya kilimo iliyo mchangiaji mkubwa wa pato la taifa imepunguziwa mgao wake kwa shilingi bilioni 7.

Kiwango hicho hakijatimiza vigezo vya makubaliano ya Malabo na Kampala ambayo ni asilimia 10 ya bajeti ya taifa.

Kwenye makadirio hayo ya bajeti,serikali inatazamia kupokea shilingi bilioni 56.91 kutoka kwa washirika wa maendeleo kama ruzuku ya masharti.

Serikali ya taifa imetengewa shilingi trilioni 2.419 kwa jumla.

Katika hatua iliyotazamwa kama kukaidi utaratibu wa gharama za juu, Waziri wa fedha John Mbadi aliwasili kwenye majengo ya bunge kwa mguu kinyume na watangulizi wake ambao wamekuwa wakiingia kwa gari aina ya Passat la kampuni ya Ujerumani ya Volkswagen.

Volksagen Passat ni gari lililo na sifa ya kuwa na ufanisi wa petroli na kulinda mazingira.

Safari ya kutokea wizara ya fedha hadi bungeni kwa mguu inachukua dakika 9.Kadhalika Waziri Mbadi alifika bungeni nusu saa kabla ya muda aliotengewa kuanza kusoma bajeti ya mwaka 2025/26.

Kabla ya bajeti mpya kusomwa,waandamanaji walikusanyika katikati ya jiji kudai haki kufuatia mauaji ya mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang’.

Polisi wakipita sehemu ambako magari yaliteketezwa kufuatia maandamano Nairobi
Polisi wakipita sehemu ambako magari yaliteketezwa kufuatia maandamano NairobiPicha: Andrew Kasuku/AP Photo/picture alliance

Wanaharakati hao walibeba mabango na kupiga mayowe wakisema bila haki hakuna bajeti.

Itakumbukwa kuwa mwaka uliopita, vijana waliandamana kupinga gharama za maisha wakati wa kusoma bajeti ya mwaka 2024/25.

Kulingana na Waziri wa Fedha John Mbadi,maandamano hayo yanaashiria kuwa wakenya wako chonjo na wanaelewa kinachoendelea hivyo basi, wizara iliamua kuwashirikisha zaidi katika bajeti mpya ya mwaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *