Haya yamesemwa Alhamis na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu lililo na makao yake New York, Human Rights Watch, HRW.
Taifa hilo maskini la Maziwa Makuu lilifanya uchaguzi wa bunge mnamo Juni 5 ambapo chama tawala cha CNDD-FDD kilipata asilimia 96 ya kura na viti vyote 100 vya bunge, kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa Jumatano.
Matokeo hayo yalipingwa kwa haraka na wagombea wa upinzani waliodai kulikuwa na wizi wa kura kupitia vitendo vya kulazimishwa kupiga kura na kuzuiwa kupata taarifa.
Shirika la HRW katika taarifa limesema limefanya mahojiano na wanaharakati, waandishi wa habari, raia na afisa wa chama tawala tawi la vijana.
Kura nyingi zaidi ya wapiga kura wlaioandikishwa
Shirika hilo linasema hao waliohojiwa wamezungumzia masuala ya kutishwa na uchakachuaji kuelekea na wakati wa uchaguzi.
Mtafiti mkuu wa Human Rights Watch katika eneo la Maziwa Makuu Clementine de Montjoye ameuelezea uchaguzi huo kama “uliokosa ushindani” akidai chama tawala kilifanya kila hila kishinde.
“Demokrasia ya Burundi imekufa, imeuliwa na chama tawala ambacho hakitaki uwajibikaji kwa watu wake na hakitaki kupingwa, licha ya hali ya uchumi kuzidi kuwa mbaya,” alisema de Montjoye. “Bila upinzani uchaguzi huu unazidi kuonyesha utawala wa kidikteta na unawasukuma Warundi chini zaidi katika mgogoro wa kiutawala.”
HRW linasema katika baadhi ya maeneo idadi ya kura zilizopigwa zilizidi idadi ya wapiga kura wlaioandikishwa.
Rais Eavriste Ndayishimiye aliingia madarakani mnamo Juni 2020 baada ya kifo cha mtangulizi wake Pierre Nkurunziza, aliyeiongoza Burundi kwa mkono wa chuma kwa miaka 15.