UNHCR: Watu milioni 122 walazimika kukimbia makwao

Ongezeko la takriban milioni 2 kutoka mwaka jana na karibu mara mbili katika muongo uliopita. Ripoti hii imetolewa kama sehemu ya Ripoti ya Mwelekeo wa Kimataifa ya UNHCR, ikieleza kuwa idadi ya watu waliolazimika kuwa wakimbizi wa nje au ndani ya nchi zao kufikia Aprili iliongezeka hadi milioni 122.1 kutoka milioni 120 mwaka uliopita.

Hata hivyo, Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, amesema kumekuwa na matumaini katika miezi sita iliyopita, ikiwemo kurejea nyumbani kwa karibu wakimbizi milioni 2 wa Syria huku taifa hilo likijaribu kujijenga upya baada ya zaidi ya muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Shirika hilo limesema Sudan, inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, imekuwa kitovu cha mgogoro mkubwa wa uhamiaji duniani, na zaidi ya watu milioni 14 wakilazimika kuhama. Nchini Syria, watu milioni 13.5 walikimbia makwao, zaidi ya milioni 10 nchini Afghanistan walihamishwa kwa lazima, na takriban milioni 8.8 kutoka Ukraine.

Ripoti hii inatolewa wakati ambapo mashirika ya kibinadamu yanakabiliwa na kupunguzwa kwa bajeti kutoka Marekani na wafadhili wa jadi wa Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *