Raundi mbili za mazungumzo ya amani mjini Istanbul kati ya Urusi na Ukraine zimeshindw akupata mwafaka wa kuvimaliza vita hivyo na kikubwa kilichokubaliwa ni ubadilishanaji wa wafungwa na kurudishwa nchini mwao kwa wanajeshi waliofariki kutokana na vita hivyo.
Na sasa shirika moja la serikali ya Ukraine limetangaza kuwa miiliya wanajeshi hao zaidi ya elfu moja imerejeshwa Ukraine. Miongoni mwa wanajeshi waliorejeshwa ni wale wlaiokuwa wakipigana katika maeneo ya Kharkiv, Lugansk, Donetsk, Zaporizhzhia na Kherson pamoja na wale waliouwawa Ukraine ilipofanya uvamizi katika eneo la Kursk nchini Urusi.
Ukraine imesema wataalam wake watazitambua maiti hizo katika kipindi cha muda mfupi.
Miili katika malori ya jokofu
Kwa siku kadhaa Urusi imekuwa ikiilaumu Ukraine kwa kutoichukuamiili ya wanajeshi wake iliyokuwa kwenye malori yenye jokofu karibu na mpakani tangu siku ya Jumamosi.
Urusi inasema iliridhia wiki iliyopita kuipa Ukraine miili ya wanajeshi 6,000 waliouwawa. Pande hizo mbili pia zilikubaliana kubadilishana wafungwa kwa kiasi kikubwa ambapo hatua za kwanza za ubadilishanaji huo zilifanyika Jumatatu na Jumanne.
Urusi imekataa miito ya usitishwaji wa mapigano bila masharti na inataka Ukraine iachie sehemu kubwa ya ardhi yake na pia iuache mpango wake wa kutaka kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, iwapo inataka amani.
Urusi pia imeendelea kuivamia miji ya Ukraine kwa makombora na ndege zisizokuwa na rubani, mashambulizi ya hivi karibuni yakifanyika usiku wa kuamkia Jumatano ambapo watu 3 walifariki dunia katika mji wa kaskazini mashariki mwa Ukraine wa Kharkiv.
Ukraine iliijibu Urusi kwa mashambulizi ya droni pia.