Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi gawio la shilingi bilioni 10.5 kwa Serikali ikiwa ni ongezeko la asilimia 600 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Gawio hilo limetolewa kutokana na faida iliyopatikana na benki hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo jumla ya gawio la shilingi bilioni 35 lilitangazwa kwa wanahisa wote wa benki hiyo. Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 30 ya hisa za NBC, hivyo inanufaika moja kwa moja na ongezeko hilo la mapato.
Katika hafla ya kitaifa ya kupokea gawio kutoka kwa mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali inamiliki hisa, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa wito kwa mashirika na taasisi zote za umma kuhakikisha yanawajibika ipasavyo kwa kulinda na kuendeleza uwekezaji wa serikali, huku akisisitiza umuhimu wa kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, ameipongeza Benki ya NBC kwa mafanikio yake na kueleza kuwa licha ya serikali kuwa na umiliki mdogo wa hisa, benki hiyo imeendelea kujiendesha kwa mafanikio makubwa. “Tumeshuhudia mabadiliko chanya na ufanisi mkubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Tukiwa na umiliki wa asilimia 30 tu, tumepokea gawio la bilioni 10.5 kwa mwaka huu, jambo linalodhihirisha uimara wa benki hii,” amesema Mchechu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi, amesema mafanikio hayo yanatokana na mkakati madhubuti wa benki katika kukuza huduma na kuboresha miundombinu ya kifedha.
#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi