Ujerumani iliwapa uraia wageni wengi mwaka 2024

Ujerumani iliweka rekodi katika historia yake kwa kuwapa watu wengi uraia mwaka 2024 kukiwa na ongezeko la asilimia 46 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Jumla ya watu 291, 955 walipata uraia wa Ujerumani huku Wasyria wakichukua sehemu kubwa ya idadi hiyo, kulingana na data zilizotolewa Jumanne na Afisi ya Takwimu ya Shirikisho.

Mshiriki wa sherehe ya kupewa uraia Ujerumani akionyesha cheti chake
Mshiriki wa sherehe ya kupewa uraia Ujerumani akionyesha cheti chakePicha: Oliver Berg/dpa/picture alliance

Afisi hiyo inasema mageuzi yaliyofanyiwa sheria ya kupata uraia Ujerumani,yalichangia pakubwa kwa ongezeko la idadi hiyo. Mwezi Juni mwaka 2024, Ujerumani ilipunguza muda anaohitaji mtu kuishi nchini humo ili kupata uraia kutoka miaka 8 hadi miaka 5.

Raia wengi wa Syria waliowasili Ujerumani kama wakimbizi mwaka 2015 na 2016 pale Kansela Angela Merkel alipowafungulia mipaka maelfu kwa mamia waliokuwa wanakimbia vita na mateso, walikuwa wametimiza vigezo vya kuwa raia mwaka 2024.

Hiyo ndiyo sababu iliyowapelekea kuwa idadi kubwa ya raia wapya. Kati ya hao waliopata uraia, asilimia 28 walikuwa Wasyria, wakifuatiwa an waturuki waliokuwa na asilimia 8, kisha Wairaki wakiwa asilimia 5, Warusi wakiwa asilimia 4 na Waafghani wakiwa na asilimia 3.

Sheria mpya ya uraia pacha Ujerumani pia inawakubalia watu kusalia na uraia wao wa awali na wakati huo huo kupata uraia wa Ujerumani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *