Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amezindua rasmi bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma. Katika uzinduzi huo, Waziri Mhagama ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inaimarisha huduma za kibingwa na kibobezi zinazotolewa na taasisi hiyo muhimu ili ziwafikie wananchi wengi zaidi nchini.
Amehimiza kuwa mafanikio ya uwekezaji katika sekta ya afya hayataonekana kama huduma hizo hazitafika kwa walengwa wenye uhitaji.
Waziri Mhagama amewakumbusha wajumbe wa bodi hiyo kwenda kuendeleza misingi mizuri iliyowekwa MOI huku wakiongeza ubunifu na mikakati bora ya kuboresha utoaji wa huduma. Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa bodi hiyo kushirikiana kwa karibu na uongozi wa MOI ili kuhakikisha kuwa huduma bora zinaendelea kutolewa kwa kiwango cha juu kwa wananchi wote, bila kujali uwezo wao wa kifedha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Dkt. Marina Njelekela, ameahidi kuwa bodi itashirikiana kikamilifu na Menejimenti ya MOI kuhakikisha taasisi hiyo inapiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amemhakikishia waziri kuwa taasisi hiyo itaendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya nchini.
#AzamTVUpdates
✍Upendo Michael
Mhariri | John Mbalamwezi