Urusi na Ukraine wabadilishana wafungwa wa kivita

Mabadilishano hayo yaliyotangazwa na pande zote mbili, ni matokeo ya mazungumzo ya ana kwa ana ya mjini Istanbul mnamo Juni 2, ambako kulifikiwa makubaliano ya kubadilishana karibu wafungwa wa kivita 1,200 kutoka kila upande pamoja na kurejesha miili ya maelfu ya waliouawa vitani.

Kurejeshwa kwa wafungwa hao wa kivita na miili ya waliouawa ni miongoni mwa masuala machache ambayo pande hizo mbili zilifanikiwa kukubaliana, wakati wakishindwa kuafikiana kwenye makubaliano mapana ya kuvimaliza vita ambavyo vimepindukia mwaka wa nne sasa.

Rais wa Ukraine VolodymVolodymyr Zelensky amesema taifa lake limepokea kundi la kwanza la wafungwa kutoka Urusi na kusema itawachukua siku kadhaa kumaliza zoezi hilo.

Hata hivyo kwa upande mwingine ameishutumu Urusi kwa mchezo mchafu wa kisiasa kuhusiana na mabadilishano hayo, baada ya pande hizo mbili kushutumiana kwa kuuchelewesha mchakato huo tofauti na walivyokubaliana kwenye mazungumzo hayo.

“Ni bahati mbaya Urusi haijatupatia orodha kamili ya maelfu ya watu kama tulivyokubaliana Istanbul. Kwa hiyo, Urusi kama kawaida yake inajaribu kucheza mchezo mchafu, kisiasa na kwenye utoaji wa taarifa. Ni muhimu kwamba kunakuwepo na matokeo. Ni muhimu watu warudishwe nyumbani. Tunaamini tutaendeleza mchakato wa kubadilishana na tunafanya kila liwezekanalo kwa ajili ya hili.”

2025 Ukraine | Vita vya Ukraine
Wafungwa wa kivita wa Ukraine wakiwa wamekumbatiana baada ya zoezi la mabadilishano kukamilikaPicha: Handout/Ukrainian Presidential Press Service/AFP

Hakuna upande ambao umeeleza ni wafungwa wangapi ambao imewaachilia hii leo, lakini Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kwa kifupi tu kwenye taarifa yake kwamba mabadilishano ya leo yamehusisha idadi sawa kutoka pande zote. Afisa wa ikulu ya Kremlin Vladimir Medinsky alisema mwishoni mwa wiki kwamba orodha ya kwanza ya wafungwa 640 imekabidhiwa kwa Ukraine.

Jeshi la Urusi limesema wanajeshi wake waliorejeshwa walipelekwa Belarus kwanza, ambaye ni mshirika wake wa karibu, ambako walikuwa wakipewa huduma ya kisaikolojia na tiba kabla ya kupelekwa Urusi kwa ajili ya msaada zaidi.

Na mapema leo, Kremlin imesema kwamba Urusi ilikuwa tayari kuheshimu makubaliano hayo na Ukraine ya kubadilishana wafungwa wa kivita pamoja na kuirejesha miili ya wanajeshi waliouawa licha ya kile ilichokisema kwamba Ukraine imeshindwa kuheshimu kikamilifu makubaliano. Ukraine lakini imekana madai hayo.

Urusi yazidi kuishambulia Ukraine

Mbali na mabadilishano hayo, pande hizo zimeendelea kushambuliana, baada ya jeshi la Ukraine kusema Urusi imeirushia droni karibu 500, hayo yakiwa ni mashambulizi makubwa zaidi la usiku mmoja tangu vita hivyo vilipoanza mwaka 2022.

Pamoja na droni hizo, Urusi pia ilirusha makombora 20 ya aina tofauti tofauti kwenye maeneo kadhaa ya Ukraine, limeongeza jeshi hilo na kusema mashambulizi yalilenga zaidi maeneo ya katikati na magharibi mwa Ukraine. 

Hata hivyo limesema mifumo yake ya ulinzi ilidungua droni 277 na makombora 19 usiku wa jana Jumapili na kudai kwamba ni droni 10 tu ama makombora yalianguka kwenye maeneo yalikolengwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *