Marekani imeanza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Sudankuanzia Juni 6, baada ya kuishutumu serikali ya nchi hiyo kutumia silaha za kemikali mwaka 2024. Hatua hiyo inajumuisha vizuizi kwa bidhaa kutoka Marekani kwenda Sudan, pamoja na kusitisha huduma za mikopo kutoka kwa taasisi za serikali ya Marekani.
Watumishi wa umma Sudan wapambana na hali ngumuMsemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tammy Bruce, amesema vikwazo hivyo vinakusudia kuiwajibisha serikali ya Sudan kwa madai hayo. Lakini wachambuzi wa kisiasa nchini Sudan wameonya kuwa vikwazo hivyo vitaathiri vibaya juhudi za ujenzi wa upya wa nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Haitham Mohammed, ni mchambuzi wa kisiasa, na anasema
“Vikwazo hivi, kwa athari zake katika sekta ya benki na mfumo wa mikopo wa Sudan, vitapunguza uwepo wa kampuni kubwa zinazohusika na ujenzi wa taasisi za serikali, kama vile miundombinu, umeme, maji, shule na hospitali.”
Mahasimu wa Sudan wakutana tena kujadili suluhu ya mzozoHata hivyo, wachumi wanasema kuwa athari halisi za vikwazo hivyo huenda zikawa ndogo, ikizingatiwa kuwa Sudan kwa sasa haina biashara ya moja kwa moja ya uagizaji kutoka Marekani wala msaada wowote wa kifedha kutoka kwa serikali ya Marekani, kama anavyobainisha mtaalamu wa uchumi Mohamed El-Nayer.
“Vikwazo vimewekwa kwa bidhaa za Marekani kwenda Sudan. Lakini kulingana na ripoti za Benki Kuu ya Sudan, hakuna uagizaji wa moja kwa moja kutoka Marekani. Kwa hiyo, hili halitaleta athari yoyote kwa kipindi kijacho. Kuhusu mikopo na fedha kutoka serikali ya Marekani, kwa sasa hakuna malipo yoyote yanayotolewa kwa Sudan kutoka kwa serikali ya Marekani wala taasisi zake.”
Wakati huo huo, serikali ya Sudan imekanusha vikali madai ya matumizi ya silaha za kemikali. Waziri wa Afya wa Jimbo la Khartoum, Fath Al-Rahman Mohammed, amesema uchunguzi wa kitaalamu haujathibitisha kuwepo kwa sumu yoyote katika miili ya waathirika.
“Vifo vingi tunavyopokea hapa vinatokana na utapiamlo na kipindupindu. Hatuna kesi za silaha za kemikali, kwani silaha ya kemikali humuua mwathirika papo hapo. Vipimo vyote tulivyofanya havijaonyesha uwepo wa sumu. Tuna maabara maalum kwa ajili ya uchunguzi huo.”
Sudan imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 2023 kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, RSF. Machafuko hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni kuyakimbia makazi yao ndani na nje ya Sudan.
Na huku vikwazo vipya vikianza kutekelezwa, Sudan inakabiliwa na changamoto kubwa ya kujenga upya taasisi muhimu, wakati mapigano na mzozo wa kibinadamu vikiendelea.