Israel yazuia boti iliyobeba wanaharakati kuingia Gaza

Wanaharakati hao walikuwa wamejipanga kupinga kampeni ya kijeshi inayoendelea ya Israel katika Ukanda wa Gaza, ambayo ni miongoni mwa mashambulizi mabaya na yenye uharibifu mkubwa tangu Vita vya Pili vya Dunia, na vikwazo vyake vya kuingia kwa misaada ya kibinadamu, ambavyo vyote vimeliweka eneo la Wapalestina lenye wakazi wapatao milioni 2 katika ukingo wa njaa.

Muungano wa Freedom Flotilla, ambao ulikuwa umeandaa safari hiyo ulisema wanaharakati hao “walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel”, wakati wakijaribu kupeleka misaada inayohitajika katika eneo hilo.

Thunberg, mwanaharakati mashuhuri wa masuala ya mazingira, alikuwa ni miongoni mwa wanaharakati 12 waliokuwamo ndani ya boti hiyo kwa jina la Madleen, ambayo ilianza safari kutoke eneo la Sicily nchini Italia wiki moja iliyopita. Greta alieleza katika mkanda mfupi wa vidio uliorekodiwa hapo kabla akisema kuwa “wanazuiliwa na kutekwa katika eneo la kimataifa la bahari”.

Israel 2025 |Wanaharakati katika boti ya Madleen
Wanaharakati wakizuiliwa na vikosi vya IsraelPicha: Israel Foreign Ministry via X/REUTERS

“Jina langu ni Greta Thunberg, na ninatoka Sweden. Ukiona video hii, tumezuiliwa na kutekwa nyara katika maji ya kimataifa na vikosi vya jeshi la Israeli au vikosi vinavyounga mkono Israeli. Ninawaomba marafiki zangu, familia na ndugu zangu wote kuweka shinikizo kwa serikali ya Sweden kuniachilia mimi na wengine haraka iwezekanavyo,” alisema Greta.

Wizara ya mambo ya nje ya Israel, imeielezea safari ya boti hiyo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kama tukio la kujionyesha na kwamba inaelekea katika fukwe za Israel na inatarajiwa kutia nanga katika bandari ya Ashdod baadae hii leo. Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa wanaharakati hao watarejea katika nchi zao na msaada huo utatumwa Gaza kwa njia iliyoanzishwa.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz aliliamuru jeshi siku ya Jumapili kuizuia boti hiyo ya Madleen kufika Gaza, akiutaja ujumbe huo wa kibinaadamu kuwa ni juhudi za propaganda za kuunga mkono Hamas.

Italien Catania 2025 | Greta Thunberg na wanaharakati wengine katika boti ya Madleen kuelekea Gaza
Greta na wanaharakati wengine katika boti ya Madleen ItaliaPicha: Freedom Flotilla Coalition/REUTERS

Uturuki na Iran zimelaani kitendo hicho cha Israel cha kuizuia boti hiyo zikisema ni “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa” na uharamia. Kundi la Hamas nalo limelaani kitendo hicho, likisema katika taarifa yake kwamba boti hiyo ilikuwa ikipelekwa katika bandari ya Ashdod ya Israel.

Israel inakabiliwa na shinikizo la kimataifa la kuruhusu msaada zaidi kuingia Gaza ili kupunguza uhaba mkubwa wa chakula na mahitaji ya kimsingi.

Wakati huo huo jeshi la Israel lilisema siku ya Jumapili kuwa limeupata na kuutambua mwili wa Mohammed Sinwar, anayedhaniwa kuwa kiongozi wa Hamas huko Gaza, katika “njia ya chini ya ardhi chini ya Hospitali ya Ulaya huko Khan Yunis”, kusini mwa Gaza.

Sinwar alikuwa mdogo wa kiongozi wa Hamas aliyeuawa Yahya Sinwar, anayeshutumiwa na Israel kwa kupanga shambulio la 2023 ambalo lilianzisha vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *