Marekani: National Guard wawasili Los Angeles bada ya vurugu

Maafisa wa Jeshi la Akiba la Marekani wameanza kuwasili katika maeneo ya maandamano katikati ya jiji la Los Angeles. Kwa mujibu wa picha za kituo cha televisheni cha ABC7, wanajeshi hao walionekana wakijipanga mbele ya jengo la Hall of Justice karibu na ukumbi wa Jiji la Los Angeles, huku wakisindikizwa na magari ya kijeshi.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, msafara wa wanajeshi pia ulipita katika kitongoji cha Paramount, eneo lililoshuhudia mapambano makali kati ya waandamanaji na maafisa wa serikali ya shirikisho, ambapo gesi ya kutoa machozi ilitumika kuwatawanya waandamanaji.

USA California - National Guard
Mgari ya kikosi cha Akiba, cha National Guard)Picha: Rich Pedroncelli/AP

Trump: “Tutaikomboa Los Angeles”

Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Rais Trump alisema ameagiza hatua za haraka “kuikomboa Los Angeles kutokana na uvamizi wa wahamiaji na kumaliza ghasia za wahamiaji.”

Alisema tayari ameagiza hatua hiyo kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth na Mwanasheria Mkuu Pam Bondi, wakishirikiana na idara nyingine za serikali.

“Utaratibu utarejeshwa, wahamiaji haramu watafukuzwa, na Los Angeles itakuwa huru tena,” aliandika Trump.

Aidha, aliwatuhumu waandamanaji kuwa ni “wapinzani wa mrengo mkali wa kushoto waliolipwa,” na kuonya kuwa kuvaa barakoa kwenye maandamano hakutaruhusiwa tena.

Aliongeza kuwa maafisa wa California wanaozuia utekelezaji wa msako wa wahamiaji wanaweza kufunguliwa mashtaka.

Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alisema wanajeshi wa Kikosi cha Ulinui wa taifa waliopelekwa Los Angeles “watasimamia sheria na utulivu kwa nguvu kubwa sana.” Aliongeza kuwa hana mpango wa kuruhusu “watu wenye vurugu” kuendeleza fujo.

Katika majibu kwa swali kuhusu uwezekano wa kutumia Sheria ya Uasi (Insurrection Act), Trump alisema: “Tunatafakari uwezekano wa kupeleka wanajeshi kila mahali. Hatutaruhusu hili litokee katika nchi yetu.”

Bernie Sanders: Marekani inapelekwa kwenye utawala wa kiimla

Seneta Bernie Sanders, mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa mrengo wa kushoto, amemshutumu Rais Trump kwa kuipeleka Marekani kwenye njia ya utawala wa kiimla.

Akizungumza na CNN, Sanders alisema: “Huyu mtu [Trump] anataka mamlaka yote. Haamini katika katiba, wala katika utawala wa sheria.”

Alisema serikali ya California wala mji wa Los Angeles hawakuomba msaada wa wanajeshi hao, lakini Trump anaamini “anaweza kufanya anavyotaka.”

Sanders aliendelea kuorodhesha vitendo vya Rais Trump vinavyoashiria kupindisha misingi ya kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na: Kuvishtaki vyombo vya habari vinavyomkosoa; kuwatesa mawakili wa mashirika yanayompinga; kuchukua hatua dhidi ya vyuo vikuu vinavyofundisha masomo asiyoyapenda; kutishia kuwaondoa majaji wanaotoa hukumu dhidi yake; na kutumia vibaya mamlaka ya Bunge la Marekani

“Hii ni hatari kubwa kwa demokrasia ya Marekani,” aliongeza Sanders.

Trump anyakua mamlaka ya Gavana Newsom

Katika hatua ya nadra, Trump amechukua mamlaka ya moja kwa moja ya usimamizi wa Jeshi la Akiba la California, akinyakua mamlaka ya Gavana wa jimbo hilo, Gavin Newsom. Kwa kawaida, magavana wa majimbo huongoza vikosi vya ulinzi wa taifa, lakini Trump ametumia kifungu cha sheria ya Title 10, kinachoruhusu Rais kuchukua udhibiti ikiwa kuna uasi au tishio la uasi dhidi ya serikali ya Marekani.

Gavana Newsom ameikosoa vikali hatua hiyo, akiitaja kuwa “ya uchochezi wa makusudi,” na kuonya kuwa inaweza kuongeza mvutano. Aidha, amewataka wananchi wa Los Angeles kutoshiriki kwenye ghasia.

Wataalamu wa sheria waonya

Profesa Erwin Chemerinsky wa Chuo Kikuu cha UC Berkeley amesema kuwa hatua hiyo “inatumia jeshi kwa ajili ya kuzuia maandamano ya kiraia,” na akaonya kuwa inatoa ishara mbaya kuhusu namna utawala wa Trump unavyokusudia kukabiliana na maandamano ya raia.

“Ni jambo la kutisha kuona serikali ikitumia jeshi kuzuia sauti za wananchi,” alisema Profesa Chemerinsky.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, hii ni mara ya kwanza katika miongo kadhaa kwa Rais wa Marekani kuchukua hatua ya kuamuru matumizi ya National Guard bila ombi la gavana wa jimbo.

Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1965, wakati Rais Lyndon B. Johnson alipoagiza wanajeshi kupelekwa Alabama kulinda waandamanaji wa haki za kiraia.

Waandaaji wa maandamano wamepanga kuendelea na maandamano katika maeneo mbalimbali ya jiji la Los Angeles, huku hali ya tahadhari ikitanda.

Mashirika ya haki za binadamu yameonya kuhusu uwezekano wa matumizi ya nguvu kupita kiasi na ukiukaji wa haki za msingi za kiraia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *