Mapema alfajiri, mahujaji walimiminika kwenye bonde la Mina, kilomita chache kutoka Makka, wakirusha mawe saba kwenye kila moja ya kuta tatu zinazowakilisha majaribu ya Shetani aliyemjaribu Nabii Ibrahim Alayhi ssalaam kutomtii Mwenyezi Mungu.
Mmoja wa mahujaji, Wael Ahmed Abdel Kader kutoka Misri, alisema waliingia Mina na ndani ya dakika tano tu wakamiliza ibada ya kupiga mawe kwenye Jamarat, akilitaja zoezi hilo kuwa rahisi na lenye utulivu.
Kwa mahujaji kama Howakita kutoka Guinea, kushiriki ibada hiyo na kusherehekea Eid akiwa Makka ni jambo la kipekee: “Niliporusha mawe nilihisi faraja kubwa. Nilijivunia sana,” alisema.
Hapo jana Alhamisi (05.06.2025), ibada ya Hijja ilifikia kilele chake kwa mahujaji kukusanyika kwenye Mlima Arafat, mahali ambapo inasadikiwa Mtume Muhammad alitoa hotuba yake ya mwisho.
Katika Msikiti wa Al-Namirah, Sheikh Salih Bin Homaid, Imam wa Msikiti huo, alitoa hotuba maalum, akiwahimiza mahujaji kuwaombea Wapalestina.
“Ee Mola, uwe pamoja na ndugu zetu huko Palestina. Ee Mola, wahurumie walio na njaa, walishe, wavalishe wasio na mavazi, wahifadhi waliokosa makazi, wape amani walioko katika hofu, na uwalinde dhidi ya maadui zao. Ee Mola, wape ushindi dhidi ya maadui zao na maadui zako kwa nguvu zako, Ewe Mwenye nguvu, Ewe Mwenye enzi.”
Tahadhari kali za kiafya na kiusalama
Kwa mara nyingine, mamlaka za Saudi Arabia zimechukua tahadhari kali za kiafya na kiusalama kufuatia janga la joto la mwaka jana lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji 1,300.
Mwaka huu, idadi ya mahujaji imeshuka ikilinganishwa na miaka iliyopita, ikiwa ni ndogo zaidi katika miongo mitatu. Wakati ibada ya Hijja ikihitimishwa, Sikukuu ya Eid al-Adha imeadhimishwa kwa hali tofauti sehemu mbalimbali duniani.
Katika Kanda ya Afrika Mashariki, maelfu ya waumini wamekusanyika katika viwanja mbalimbali kwa ajili ya Sala ya Eid. Nchini Kenya, waumini wa dini ya Kiislamu walijumuika katika viwanja vya shule ya Msingi ya Kilimani na Uwanja wa Tononoka mjini Mombasa na kwingineko, ambapo viongozi wa dini walitoa wito wa mshikamano na kusaidia wasiojiweza.
Nchini Tanzania, swala rasmi inatarajiwa kuswaliwa hapo kesho, lakini baadhi ya waumi wameungana na jumuiya ya kimataifa na kuswali swala yao hii leo katika viwanja na misikiti mbalimbali.
Nchini Uganda, mamia ya waumini wamekusanyika katika Msikitu Mkuu mjini Kampala wakiungana katika sala hiyo, wakiomboleza pia mateso yanayowakumba Waislamu wa Palestina. Katika miji yote hii, ujumbe umekuwa mmoja, amani, mshikamano na kujitolea kwa ajili ya jamii.