Hamdok amesema mafanikio ya kijeshi hayatamaliza vita Sudan

Hamdok amepuuza hatua ya jeshi la nchi hiyo kuunda serikali mpya, akizitaja juhudi hizo kuwa ni “za kughushi,” na kuonya kwamba ushindi wa karibuni wa kijeshi hauwezi kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na shirika la habari la Associated Press pembeni mwa kongamano la utawala la Mo Ibrahim mjini Marrakech, Morocco, Hamdok alisema hakuna ushindi wa kijeshi unaoweza kuleta suluhu ya kudumu kwa mgogoro wa Sudan.

“Kama Khartoum imetekwa au haijatekwa, hilo halina maana yoyote,” alisema. “Hakuna suluhisho la kijeshi kwa vita hivi. Hakuna upande utakaoibuka mshindi wa moja kwa moja.”

Hamdok alihudumu kama Waziri Mkuu wa kwanza wa kiraia baada ya miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi nchini Sudan. Alijiuzulu Januari 2022 baada ya kipindi cha misukosuko kilichojumuisha kupinduliwa na kurejeshwa madarakani kwa shinikizo la kimataifa.

Vita vilizuka mwaka uliofuata baada ya majenerali wawili kugombea madaraka, na hadi sasa vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 24,000 huku wengine takriban milioni 13 wakikimbia makazi yao – milioni 4 kati yao wakivuka mipaka ya kimataifa.

Licha ya jeshi kurejesha udhibiti wa Khartoum mwezi Machi, pamoja na maeneo jirani, mapigano yameendelea. Kikosi cha RSF chenye mizizi katika kundi hatari la Janjaweed, kimejipanga upya katika ngome yao ya Darfur na kufanya mashambulizi mapya maeneo mengine kama Kordofan.

“Serikali yoyote inayoanzishwa sasa ni ya bandia na haina uhalali”

Abdalla Hamdok amesisitiza kwamba jaribio lolote la kuunda serikali nchini Sudan kwa wakati huu halitakuwa na maana na kuongeza kuwa amani ya kudumu haitapatikana kama mzizi wa mzozo hautashughulikiwa kwanza
Abdalla Hamdok amesisitiza kwamba jaribio lolote la kuunda serikali nchini Sudan kwa wakati huu halitakuwa na maana na kuongeza kuwa amani ya kudumu haitapatikana kama mzizi wa mzozo hautashughulikiwa kwanzaPicha: AFP/Getty Images

Hamdok amesema hatua ya kuteua Waziri Mkuu mpya, Kamil al-Taib Idris, haitabadili hali ya mambo, akisisitiza kuwa “serikali yoyote inayoanzishwa sasa ni ya bandia na haina uhalali.”

Kwa mujibu wa waziri mkuu huyo wa zamani, suluhu ya kweli inapaswa kuanzia kwa kusimamisha mapigano na kuanzisha mchakato wa kuleta utawala wa kiraia na kidemokrasia, huku akisisitiza haja ya kushughulikia mizizi ya mzozo huo kama vile ukosefu wa usawa wa maendeleo, mgawanyiko wa kijamii na nafasi ya dini katika serikali.

Hamdok pia alikosoa mataifa ya nje kwa kuchochea vita kwa kutoa silaha kwa pande zinazopigana, ingawa aliepuka kuushutumu moja kwa moja Umoja wa Falme za Kiarabu(UAE) kwa madai ya kuisaidia RSF, akisema lawama zinapaswa kuelekezwa kwa wote wanaounga mkono upande wowote wa kivita.

“Tungependa kuona yeyote anayesambaza silaha kwa upande wowote anasitisha mara moja”, alisema Hamdok, akionya kuwa kuendelea kwa usaidizi wa kivita kutoka nje kunaifanya Sudan kuendelea kuwa uwanja wa mapambano ya madola ya kigeni badala ya kuwa nchi ya amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *