Urusi na Ukraine zashindwa kuafikiana

Duru hiyo ya pili ya mazungumzo ya amani ya moja kwa moja imekamilika kwa pande zote mbili kutofikia makubaliano yeyote ya kumaliza mzozo kati yao wenye zaidi ya miaka mitatu. Maafisa wamesema jambo pekee ambalo pande hizo mbili zimekubaliana ni kukubali kubadilishana wafungwa wa kivita na miili ya askari waliopoteza maisha katika uwanja wa mapambano.
Duru zinasema wajumbe wamekubaliana kubadilishana miili 6,000ya askari waliouawa na kuunda tume ya kubadilishana askari waliojeruhiwa vibaya.

Ujumbe wa Ukraine umesema Urusi iliwasilisha hati ya masharti ya makubaliano yatakayomaliza uhasama katika meza ya mazungumzo.

2025 I Uturuki I Urusi I Ukraine
Urusi na Ukraine katika meza ya mazungumzo mjini Istanbul, UturukiPicha: Alexander Ryumin/ZUMA Press/IMAGO

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov, ambaye aliongoza ujumbe wa nchi yake amewaambia waandishi wa habari kwamba maafisa wa Kyiv watahitaji siku kadhaa kulipitia pendekezo hilo na kuamua juu ya mustakabali wake.

Ukraine yenyewe imependekeza mazungumzo mengine kati yao na Urusi yafanyike kati ya Juni 20 na Juni 30.

Urusi yatoa masharti yake

Baada ya mazungumzo hayo, mashirika ya habari ya serikali ya Urusi Tass na RIA Novosti yamechapisha taarifa kwamba pendekezo la Urusi linapendekeza kuwa Ukraine iondoe vikosi vyake kutoka kwenye mikoa minne ambayo Urusi ambayo ilitwaa mnamo Septemba 2022lakini ambayo haijafanikiwa kuidhibiti kikamilifu kwa sharti kusitisha mapigano.

Pendekezo hilo linaisisitiza Ukraine pia kusitisha juhudi zake za kuomba na kupokea silaha za kijeshi kutoka kwa nchi za magharibi na kupiga marufuku uwepo wowote wa kijeshi wa nchi nyingine katika ardhi yake.

Urusi I Ukraine
Ujumbe wa Urusi katika meza ya mazungumzo kati yao na UkrainePicha: Murad Sezer/REUTERS

Pendekezo hilo linaenda mbali zaidi kwa kuitaka Ukraine ikomeshe sheria ya kijeshi na kufanya uchaguzi, ambapo baada ya hapo, nchi hizo mbili zinaweza kutia saini ya mkataba wa amani wa kina ambao pia utaifanya Ukraine kutangaza kutoegemea upande wowote na kuachana na mpango wake wa kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO, kuweka ukomo wa ukubwa wa jeshi lake na kuitambua lugha ya Kirusi kama moja ya lugha rasmi nchini humo.

Hata hivyo, Ukraine na nchi za magharibi ziliyakataa matakwa hayo hapo awali kutoka kwa Urusi.

Juhudi zinazoongozwa na Marekani za kushinikiza pande hizo mbili kukubali usitishaji mapigano zinaonekana kugonga mwamba hadi sasa.

Na maoni ya hivi majuzi ya viongozi wakuu katika nchi zote mbili yanaonyesha bado kuna ugumu katika kufikiwa kwa makubaliano ya amani. 
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *