Kura ya maoni iliyofanywa na vituo vitatu vikuu vya televisheni vya Korea Kusini – KBS, MBC na SBS imeonyesha kuwa Lee anatabiriwa kupata 51.7% ya jumla ya kura zilizopigwa na kumshinda mgombea mkuu wa kihafidhina Kim Moon Soo aliyejipatia 39.3% ya kura.
Raia wa Korea Kusini wamchagua rais mpya kwenye uchaguzi wa mapema
Lee anaonekana kunufaika pakubwa kutokana na ghadhabu kubwa ya umma iliyosababishwa na hatua hiyo ya Yoon ya kutangaza sheria za kijeshi mnamo mwezi Disemba mwaka jana na kupelekea kutimuliwa madarakani na bunge.
Wakati matokeo ya kura hiyo yalipotangazwa, wafuasi wa chama cha Democratic walishangilia kwa shangwe kwenye ukumbi wa sherehe, huku wakiliimba jina la Lee. Katika makao makuu ya chama cha Kim, wabunge walikuwa kimya.
Upigaji kura ulianza mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, majira ya Korea Kusini, katika vituo 14,295 vyakurakote nchini humo na kufungwa saa mbili usiku. Takriban 80% ya wapiga kura milioni 44.4 walishiriki katika zoezi hilo . Haya ni kulingana na hesabu ya kura inayoendelea. Hii ni mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya wapiga kura kujitokeza kwenye uchaguzi wa urais nchini Korea Kusini na imeonyesha nia ya umma ya kuuvuuka mtikisiko uliopo wa kisiasa.
Lee awaomba wapiga kura kumchagua
Katika chapisho kwenye mtandao wa Facebook mapema Jumanne, Lee, ambaye chama chake cha Democratic kiliongoza juhudi za kisheria za kumuondoa Yoon madarakani, alitoa wito kwa wapiga kura kutoa kile alichokiita hukumu kali na thabiti dhidi ya wahafidhina juu ya sheria ya kijeshi.
Rais wa mpito wa Korea Kusini atangaza kujiuzulu
Katika moja ya hotuba zake za mwisho za kampeni, Lee alisema kuwa ushindi wa Kim utamaanisha kurejea madarakani kwa vikosi vya uasi, kuharibiwa kwa demokrasia na kubinywa kwa haki za binaadamu. Pia aliahidi kufufua uchumi, kupunguza ukosefu wa usawa na migawanyiko ya kitaifa huku akiwataka wananchi kumpigia kura.
Kwa upande wake, Kim, waziri wa zamani wa ajira chini ya uongozi wa Yoon, alionya kwamba ushindi wa Lee utamruhusu kutumia nguvu nyingi, kuanzisha kisasi cha kisiasa dhidi ya wapinzani na kutunga sheria za kumlinda dhidi ya matatizo mbali mbali ya kisheria kwa sababu chama chake tayari kinalidhibiti bunge.